Siasa

Mbunge akanganya Kalonzo kuhusu msimamo wa Wiper

February 19th, 2018 2 min read

Mbunge wa Mwingi ya Kati, Bw Gideon Mulyungi. Picha/ Maktaba

BONFACE MWANIKI na BEN MATHEKA

Kifupi:

  • Bw Mulyungi asema Wiper iko tayari kuhama Nasa wakati wowote iwapo ODM itaendelea kumkosea heshima Bw Musyoka
  • Asema sharti viongozi wa ODM wakome kumtusi Bw Musyoka kwa kuwa haikuwa lazima Kalonzo kuhudhuria “uapisho” huo
  • ODM kimekuwa kikitenga vyama vingine vya muungano huo na hiyo ndiyo sababu ilifanya Wiper kuandikia barua Spika wa Bunge

MBUNGE wa Mwingi ya Kati, Gideon Mulyungi mwishoni mwa wiki alionekana kumkanganya kinara wake katika chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka kuhusu msimamo wa chama hicho katika Muungano wa NASA.

Mnamo Jumamosi Bw Mulyungi aliwaambia wanahabari nyumbani kwake Mwingi kuwa Wiper iko tayari kuhama Nasa wakati wowote iwapo viongozi wa ODM wataendelea kumkosea heshima Bw Musyoka.

Lakini akizungumza jana katika kaunti ya Kilifi, Bw Musyoka alikariri kuwa vinara wa NASA wameungana na kuwa ni Jubilee inayobuni madai ya mgawanyiko katika muungano huo wa upinzani.

Wiki iliyopita, Bw Musyoka alionekana kuwa na msimamo tofauti alipotisha kuwa Wiper inaweza kuondoka NASA iwapo viongozi wake hawataheshimiwa na wenzao.

Bw Mulyungi alieleza kuwa hawajaridhishwa na kukosewa heshima kwa kiongozi wao Bw Musyoka na baadhi ya viongozi wa ODM tangu alipokosa kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa Raila Odinga kama “rais wa wananchi” mnamo  Januari 30.

Alisema sharti viongozi wa ODM wakome kumtusi Bw Musyoka akieleza kuwa haikuwa lazima kwake kuhudhuria “uapisho” huo uwanjani Uhuru Park.

 

Furaha ya kunguru

“Tunajua viongozi wa Jubilee wanameza mate wanapoona uwezekano wa kuvunjika kwa NASA wakidhani kuwa tunaweza kujiunga nao.

Ndugu zetu wa ODM wanafaa kuwa waangalifu, la sivyo tutawaachia muungano huo wakiwa na kiongozi wao tuone vile watakavyoendelea kivyao,” akasema Bw Mulyungi.

Kuhusu kugawana viti vya kamati za bunge, Bw Mulyungi alisema ODM kimekuwa kikitenga vyama vingine vya muungano huo na hiyo ndiyo sababu ilifanya Wiper kuandikia barua Spika wa Bunge kutaka mbunge wa Borabu Ben Momanyi kuwa mwanachama wa Tume ya Huduma ya Bunge.

ODM kiliwasilisha majina matatu ya wanachama hicho bila kushirikisha wale wa vyama vingine vya NASA, jambo analosema linaweza kusambaratisha muungano huo.

“Ndugu zetu katika ODM wanachochea mgawanyiko mkubwa katika NASA kwa sababu hatutakubali waendelee kutudhulumu ilhali kulingana na mkataba wa muungano huo tuko sawa,” alionya mbunge huyo.

Alisema Bw Musyoka sio mwoga na yuko tayari kula “kiapo” mradi tu wafuasi wake wanaunga mkono hatua hiyo.

Habari zaidi na BENSON MATHEKA