Habari MsetoSiasa

Mbunge akejeli wenzake kwa kumpigia debe Ruto

April 8th, 2018 1 min read

Na KAZUNGU SAMUEL

MBUNGE wa Ganze katika Kaunti ya Kilifi Bw Teddy Mwambire Jumamosi aliwakashifu wabunge wenzake ambao wameanza kumpigia debe naibu wa rais William Ruto kumrithi Rais Kenyatta mnamo 2022.

Akiongea katika shule ya upili ya Godoma baada ya kuhudhuria kikao kuhusu uzinduzi zoezi la usoroveya wa mashamba, Bw Mwambire alisema ni wananchi pekee wa Pwani ambao wanaweza kutoa mwongozo wa ni nani anaweza kuwania Urais 2022.

“Nimekuwa nikiangalia jinsi baadhi ya wabunge wameanza kumpigia debe Bw Ruto kuwa Rais lakini nimegundua hiyo yote ni katika harakati za kujitakia makuu. Yule ambaye anaweza kusema hilo ni mkazi wa Pwani na bado hajafanya uamuzi,” akasema Bw Mwambire.

Mbunge huyo ni mkosoaji mkuu wa sera za serikali ya Jubilee na vile vile mshirika wa karibu wa gavana Amason Kingi(Kilifi).