Habari MsetoSiasa

Mbunge akemea wanaohoji ziara za rais kwa Mzee Moi

August 7th, 2018 2 min read

Na JOSEPH WANGUI

MBUNGE wa Mathira, Bw Rigathi Gachagua, amesuta viongozi wanaohusisha ziara zinazofanywa mara kwa mara na Rais Uhuru Kenyatta kwa Rais Mstaafu Daniel arap Moi na siasa za 2022.

Hatua yake imetokana na jinsi baadhi ya wanasiasa wanavyoshuku kuwa ziara hizo zinahusiana na uchaguzi wa urais wa 2022.

“Moi ni raia mheshimiwa katika nchi hii na ana haki ya kutunzwa na watu wengine wote wadogo wake kiumri ambao wako uongozini. Rais Kenyatta anapomtembelea, hiyo ni tabia njema,” akasema Bw Gachagua.

Alisema Bw Moi anahitaji zaidi kutembelewa, hasa wakati huu ambapo hayuko katika mstari wa mbele kushiriki kwa masuala ya kitaifa.

“Ziara za Rais Kenyatta Kabarak hufuata tamaduni za Kiafrika kutembelea wagonjwa. Ni tabia mbovu kwa Wakenya kushuku kile wanachojadili,” akasema Bw Gachagua.

Aliomba Wakenya wamruhusu rais kufanya kile anachotaka ikiwemo kujumuika na kutembelea yeyote anayetaka.

“Hakuna vile rais atawaambia kila kitu anachofanya. Hafai kuhojiwa kuhusu kwa nini alimsalimia mtu huyo na si yule mwingine. Hiyo ni kukosa adabu,” akasema mbunge huyo, ambaye ni msaidizi wa zamani wa rais.

Alipoulizwa kwa nini Rais Kenyatta hajakuwa akimtembelea Rais Mstaafu Mwai Kibaki jinsi anavyomtembelea Bw Moi, mbunge huyo alisisitiza Wakenya wakome kumchunguza rais.

“Hakuna sheria inayosema unapomtembelea Moi ni lazima pia umtembelee Kibaki. Lazima rais apewe uhuru wa kufanya atakavyo,” akasema.

Bw Gachagua alipuuzilia mbali wakosoaji wa ziara hizo za Kabarak na kusema hizo huwa ni ziara za kibinafsi.

Alisema Wakenya wanaweza kumhoji rais kuhusu masuala rasmi kama vile anavyotumia rasilimali za umma lakini si kuhusu ziara zake kwa Mkenya yeyote au marafiki wake.

Ziara za Rais Kenyatta nyumbani kwa Bw Moi zilizidi kutazamwa kisiasa wakati naibu wake, Bw William Ruto, alipozuiliwa kuingia katika boma hilo hivi majuzi alipotaka kumjulia hali rais huyo mstaafu.

Bw Ruto na Seneta wa Baringo Gideon Moi, ambaye ni mwanawe rais mstaafu ni mahasimu wa kisiasa katika eneo la Rift Valley.

Kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusiana na jinsi ambavyo rais Kenyatta amekuwa akimtembelea Mzee Moi mara kwa mara.

Wengi wanaamini kuwa huenda hiyo ikawa ishara tosha kwa Bw Ruto kwamba, azma yake ya kutaka urais huenda ikatumbukia nyongo.

Tayari kumeibuka majaribio ya kutaka Bw Ruto na manaibu magavana waliohudumu kwa vipindiviwili wasiwanie nyadhifa za juu.