Mbunge alaani hatua ya wakazi kuweka uchawi mbele kuliko elimu Pwani

Mbunge alaani hatua ya wakazi kuweka uchawi mbele kuliko elimu Pwani

NA KALUME KAZUNGU

MBUNGE wa Kaloleni, Bw Paul Katana, amelaani hatua ya baadhi ya wakazi wa eneo hilo wanaodaiwa kushirikiana kushambulia wazee kwa madai kuwa ni wachawi.

Bw Katana alisema ni aibu kwa wakazi kushirikiana na hata kuchangisha pesa za kutafuta wauaji, ilhali wanapotakikana kuja pamoja kwa maslahi muhimu kama vile elimu ya watoto wao, huwa wanadai hawana uwezo wa kifedha.

Akizungumza katika eneobunge lake, alisisitiza haja ya sheria kutumika kikamilifu ili kukabiliana na wahusika wa mauaji ya wazee kwa tuhuma za uchawi.

“Ni aibu kubwa kama mimi mjumbe wa Kaloleni ninaambiwa mheshimiwa kazi yenu ni kuua watu. Hii hali nataka iishe. Cha kushangaza ni kwamba pesa za kupeana ili mtu auawe huwa mnapata, lakini mnashindwa na kuchanga pesa za kuwasomesha watoto. Ashindwe shetani!” akasema Bw Katana.

Mbunge wa Kaloleni Paul Katana. PICHA | MAKTABA

Kaunti ya Kilifi ni mojawapo ya nyingine nchini ambapo wahalifu wamekuwa wakiwaangamiza wazee kila kukicha kwa madai kuwa ni wachawi.

Uchunguzi huwa umebainisha kuwa baadhi ya wazee hao huuawa na jamaa zao hasa vijana ambao hutaka kurithi sehemu zao za ardhi au magenge yanayotaka kunyakua ardhi.

Naibu Kamishina katika eneobunge la Kaloleni, Bw Mugo Kishiri, aliwatahadharisha wakazi dhidi ya kuendeleza mauaji aina hiyo.

Bw Kishiri alisema wazee wanne waliuliwa eneo hilo wiki iliyopita, na kuongezea idadi ya wengine wengi ambao wamekuwa wakiuliwa mara kwa mara.

“Wazee ni lazima waheshimiwe. Mzee akipata mali kidogo, vijana wanaanza kusema ni mchawi. Mzee akikataa kutoa au kugawanya shamba wanasema ni mchawi. Hiyo tabia nataka ikome kabisa hapa. Na yule ambaye tutapata akijihusisha na tabia hii sheria haitamsaza,” alisema Bw Kishiri.

Wakati huo huo, maafisa wa usalama katika Kaunti ya Kilifi wametoa wito kwa wakazi na wanasiasa kuhakikisha wanadumisha amani wakati wote wa kipindi cha uchaguzi.

Afisa mkuu wa polisi eneobunge la Kilifi Kaskazini, Bw Jonathan Koech, alikariri kuwa wananchi wengi huwa wanatumiwa na wanasiasa kuvunja sheria wakati wa uchaguzi.

Akizungumza na Taifa Leo mjini Kilifi, Bw Koech aliwataka wanasiasa kufanya kampeni zao kwa njia ya amani bila kutoa matamshi ya chuki.

“Sisi tupende amani tusieneze siasa ya ukabila,” alisema Bw Koech.

Kwa upande wake, naibu kamishna katika eneobunge la Kilifi Kaskazini, Bw Geoffrey Tunai, aliwataka vijana kutokubali kutumika vibaya na wanasiasa.

Hata hivyo, Bw Tunai ameahidi kushirikiana na wenyeji wa eneo hilo ili kuhakikisha usalama unaimarika zaidi wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Tunajua kwamba tunaenda wakati wa siasa na vijana wetu wasitumike na wanasiasa kutoa fujo na kuharibu amani. Tufanye kazi pamoja na kama ni kufanya siasa ufanye kwa amani hakuna kuchokozana ama kutusi mwenzako ndio amani iwe,” alisema Bw Tunai.

Aidha, afisa huyo wa utawala alisema wameweka mikakati kabambe ya kuhakikisha hakushuhudiwi visa vyovyote vya utovu wa usalama eneo hilo kipindi hiki na hata baada ya uchaguzi.

You can share this post!

Nema yakiri Bahari Hindi yachafuliwa, hatua kuchukuliwa

TAHARIRI: Serikali iwape wakimbizi wa Mau makazi

T L