Habari Mseto

Mbunge Ali Mbogo awataka wasichana wa shule wajiepushe na ngono kuulinda utu wao

October 19th, 2020 1 min read

Na WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Kisauni Ali Mbogo amewaonya wasichana kuepuka mimba za mapema huku akisisitiza umuhimu wa kutilia maanani elimu.

Aliwataka wanafunzi hao kuwekeza katika ujuzi wao na elimu ili kuboresha maisha yao.

“Kama una talanta katika spoti hakikisha unakuwa mweledi. Tucheze boli mpira lakini tusibebe ‘boli’ mimba. Upo wakati utaweza kubeba mimba lakini kwa sasa zingatia elimu na talanta yako. Huu ndio wakati mwafaka wa kutia bidii,” alisema Bw Mbogo.

Aliwaonya wasichana hao dhidi ya kukubali kutongozwa na wavulana na kuharibu maisha yao.

“Nawaomba mjichunge; tumesikia changamoto zenu na tuko hapa kuwasaidia. Tutawapa vifaa vya kuboresha talanta zenu,” aliahidi.