Habari MsetoSiasa

Mbunge amlipia karo mvulana aliyefika shuleni na sabuni pekee

January 15th, 2020 1 min read

Na IAN BYRON

MWANAFUNZI wa kidato cha kwanza ambaye alifika Shule ya Upili ya Kanga inayopatikana katika Kaunti ya Migori akiwa na sanduku na sabuni pekee sasa ana sababu ya kufurahi baada mbunge mteule Dennitah Ghati kumlipia karo ya Sh53,000 na kumnunulia bidhaa za matumizi shuleni.

Masaibu ya Lewis Otieno, 13 anayetoka Kaunti jirani ya Homabay yaliangaziwa na runinga ya NTV Jumatatu alipofika shuleni akiwa na mamake licha ya kukosa karo na viatu.

Bw Otieno aliteuliwa ili ajiunge na shule hiyo maarufu baada ya kupata alama 391 katika mtihani wa KCPE.

“Nilimshawishi mamangu anisaidie nifike shuleni na kwa kuwa hakuwa na pesa za nauli, alilazimika kukopa kutoka kwa rafikiye katika kituo cha kibiashara cha Pala. Hivyo ndivyo safari yetu ilianza,” akaeleza Taifa Leo Jumatatu.

“Sitaki kurudi nyumbani na nitasalia hapa shuleni kwa sababu hata nikirejea hakuna kitakachobadilika. Nitasalia hapa shuleni na msaada wowote utanipata hapa. Tayari nimeruhusiwa kujiunga na shule hii na naomba msaada wa wasamaria mema,” akaongeza.

Bi Ghati ambaye aliyemtembelea mvulana huyo jana, alisema alizidiwa na hisia baada ya kusikia masaibu yake ndipo akachelewesha safari yake ya kuelekea Nairobi ili kumsaidia.

“Nilikuwa nadondokwa na machozi nilipotazama simulizi yake kwenye vyombo vya habari,” akasema.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Michael Ogweno naye alitaja kusikitishwa na hali ya mvulana huyo ndiyo maana hakumfukuza pamoja na mamake hata kama hakuwa na karo.