NA GEORGE MUNENE
MBUNGE wa Afika Mashariki (EALA), Bi Winnie Odinga, jana Jumatano alishambuliwa vikali kwa kukosa kuhudhuria mkutano uliotishwa na Rais William Ruto katika ikulu ya Nairobi.
Mbunge wa Manyatta, Gitonga Mukunji alisema kwamba Bi Odinga alikosea kwa kususia mkutano huo ulionuiwa kujadili masuala yanayohusu Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema kuwa Bunge la Taifa litaanza mchakato wa kumvua Bi Odinga kiti chake kwa madai ya kuwa na tabia mbaya.
“Bunge la Taifa litamuita Bi Odinga aeleze kwa nini hakuhudhuria mkutano muhimu ulioitishwa na Rais,” aliambia wanahabari katika ofisi ya eneo bunge lake mjini Embu.
Alisema kwamba Bi Odinga alichaguliwa na wabunge wa upinzani na wengi kutoka Kenya Kwanza kuwakilisha maslahi ya Wakenya katika Bunge la Afrika Mashariki na anafaa kuchukua majukumu yake kwa umakini.
“Wanachama wote wa EALA walienda na kukutana na Rais na Waziri wa Ukanda wa Afrika Mashariki na walikuwa hapo kupatiwa mamlaka ya kusimama kama nchini katika masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini Bi Odinga hakuwepo. Ni aibu tunajichukulia kwa mipaka ya kisiasa hata baada ya uchaguzi kupita,” alisema Bw Mukunji.
Subscribe our newsletter to stay updated