Habari Mseto

Mbunge aonya dhidi ya miradi hewa kuanzishwa na kukwama

April 4th, 2019 1 min read

Na David Muchui

MBUNGE wa Tigania Magharibi John Mutunga ameonya wasimamizi wa Hazina ya Ustawishaji wa Maeneobunge (CDF-NG) katika sehemu hiyo dhidi ya kuanzisha miradi ambayo haitamalizika katika kipindi cha mwaka mmoja.

Akiongea alipokuwa akitoa Sh29.6 milioni za ufadhili wa masomo ya

wanafunzi wa shule za upili na vyuo, Bw Mutunga alisema ameweka mikakati ya kuhakikisha kuwa miradi inayoanzishwa na hazina hiyo inakamilishwa ndani ya mwaka mmoja.

Alionya maafisa wa hazina ya CDF-NG ambao wamekuwa wakiwalipa wanakandarasi ambao hawajakamilisha miradi kuwa watachukuliwa hatua.

“Tulibaini kwamba wakandarasi wamekuwa wakilipwa fedha zao zote kabla ya miradi kukamilika. Hali hiyo imesababisha miradi mingi, ukiwemo ujenzi wa madarasa, kukwama,” akasema.

Mbunge huyo alisema wadi ya kujifungulia na madarasa ni miongoni mwa miradi iliyokwama.