Habari MsetoSiasa

Mbunge aonya kuhusu siasa za migawanyiko

November 14th, 2019 1 min read

JOSEPH OPENDA na MARGARERT MAINA

MBUNGE wa Bahati, Bw Kimani Ngunjiri ameonya kuhusu uendelezaji wa siasa za udhibiti wa maeneo fulani nchini na wanasiasa, akionya kuwa huenda zikaigawanya nchi.

Akihutubu mjini Nakuru Jumatano, Bw Ngunjiri alisema kwamba siasa hizo, ambazo zinaendeshwa na chama cha ODM ndizo chanzo cha ghasia zilizotokea kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika katika eneobunge la Kibra.

Mbunge huyo alikashifu wito uliotolewa na wabunge wa ODM kwa wafuasi wao kutowaruhusu wanasiasa wengine kuyazuru, akiutaja kama kikwazo cha juhudi za kuleta umoja na kuiunganisha nchi.

Alisema kuwa semi hizo hazifai, kwani lengo lake kuu ni kuwatishia baadhi ya wanasiasa dhidi ya kuendesha kampeni zao katika maeneo hayo.

“Kenya ni nchi huru kwetu sote. Tunapaswa kupendana licha ya tofauti zetu. Ikiwa kila mmoja atachukua mwelekeo uliodhihirishwa na ODM katika eneobunge la Kibra, basi tutakuwa na matatizo mengi kama nchi,” akasema.Alionya kwamba ikizingatiwa kuwa kaunti ya Nakuru ina jamii nyingi, huenda ikaathirika sana, ikiwa kila kiongozi atalinda eneo alikochaguliwa.

Mbunge huyo, ambaye anaegemea upande wa wale wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto, alisema kwamba viongozi waliochochea ghasia za Kibra wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alimlaumu Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i na Katibu wa Wizara Karanja Kibicho kwa madai ya kuwapendelea wale waliohusika kwenye ghasia hizo.

“Ningetaka kumwambia Dkt Matiang’i na Dkt Kibicho kukoma kuwapendelea baadhi ya watu katika utekelezaji wa sheria. Ni vipi Kuwa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kufikia sasa ilhali waliohusika wamekuwa wakisema wazi walichochea ghasia hizo?” akashangaa.