Mbunge apendekeza kutathminiwa kwa sheria za uchaguzi kukomesha kampeni za mapema

Mbunge apendekeza kutathminiwa kwa sheria za uchaguzi kukomesha kampeni za mapema

Na SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Kiminini, Chris Wamalwa amependekeza kutathminiwa kwa sheria za uchaguzi ili kuzuiwa wanasiasa kushiriki kampeni za mapema.

Licha ya kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haijatangaza kuanza rasmi kwa kampeni kufuatia uchaguzi mkuu 2022, wanasiasa wameanza kuandaa mikutano ya umma kusaka kura.

Wakiongozwa na Naibu wa Rais, William Ruto, kinara wa ODM, Raila Odinga na viongozi wa One Kenya Alliance (OKA), mrengo unaojumuisha Musalia Mudavadai (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetangula (Ford-Kenya) na Gideon Moi (KANU), wamekuwa wakizuru maeneo mbalimbali nchini katika kile kinaashiria kutafuta kura kumrithi Rais Uhuru Kenyatta mwaka ujao.

“Inashangaza kuona walioko serikalini, wakiongozwa na Rais na naibu wake, na kiongozi wa ODM ndio wanaongoza kampeni hata kabla IEBC kuruhusu kuanza,” Bw Chris akasema, akizungumza jijini Nairobi.

IEBC inapotangaza rasmi kampeni kung’oa nanga, inaruhusiwa kuadhibu kisheria wanasiasa wanaokiuka kanuni za uchaguzi, ikiwemo wanaochochea fujo na vurugu kuzuka. Kufuatia kampeni zinazoendelezwa na baadhi ya viongozi na wanasiasa, ghasia zimezuka suala ambalo linaibua hali ya wasiwasi kuhusu uchaguzi wa 2022.

Mbunge huyo anapendekeza sheria za uchaguzi kutathminiwa, ili kuipa IEBC mamlaka zaidi kuadhibu wachochezi wa vurugu hata kabla kutangaza kampeni kuanza. “Kwa sasa tume yetu ya uchaguzi haina mamlaka kwa sababu kipindi cha kuruhusu kampeni zing’oe nanga hakijawadia,” Dkt Chris akasema.

Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC), imetoa orodha ya baadhi ya maeneo ambayo huenda yakashuhudia ghasia kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu. Yanajumuisha, Nairobi, Kisumu, Eldoret, Mombasa na Nakuru.

Kauli ya Bw Chris Wamalwa imejiri siku moja baada ya Naibu Rais kudai mikutano ya umma ambayo amekuwa akiandaa maeneo tofauti nchin “ni ya kukagua miradi ya maendeleo ya serikali na kuizindua”.

Dkt Ruto aidha alisema hajaanza kampeni, katika azma yake kuwania kuingia Ikulu 2022, matamshi ambayo yameonekana kuwa kinaya. Amekuwa akitumia majukwaa ya mikutano ya umma kushambulia wapinzani wake, sawa na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Kwa watumishi wa umma wanaomezea nyadhifa za kisiasa, wanatakiwa kujiuzulu miezi sita kabla ya uchaguzi, hii ikiwa na maana kuwa watalazimika kuchukua hatua hiyo Februari 2021. Kwa mujibu wa Katiba ya sasa, iliyozinduliwa 2010 na kuanza kutumika 2013, uchaguzi unapaswa kufanywa mwezi Agosti, kila baada ya miaka mitano.

You can share this post!

Kang’ata ajitetea kuhusu mchango alioaibishwa na Naibu...

Wabunge kusafiri Denmark kunoa bongo kupitisha mswada wa...

T L