Habari Mseto

Mbunge apendekeza naibu gavana awe na mamlaka zaidi

November 7th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KAUNTI ya Kiambu inastahili kuwa na mwongozo unaofaa ili iweze kupiga hatua kimaendeleo.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alisema kutokana na kushtakiwa kwa gavana Ferdinand Waititu kugusiana na tuhuma za ufisadi, naibu gavana anapata wakati mgumu kuendesha maswala ya kaunti.

“Wakati mwingi utapotea katika kaunti hii kwa sababu shughuli nyingi zitakwama ikizingatiwa kwamba naibu gavana ana nafasi ndogo ya kutekeleza wajibu wake,” alisema Bw Wainaina.

Hata hivyo, alipendekeza kuwa ni vyema kuwe na sheria maalum inayompa naibu gavana nafasi ya kuendesha kazi za gavana bila kuwa na vikwazo fulani.

“Iwapo kutakuwa na sheria hiyo ya kumpa naibu gavana ruhusa ya kutekeleza majukumu yote bila shaka kaunti itaweza kupiga hatua zaidi,” alisema Bw Wainaina, na kuongeza miaka mitatu ambayo imesalia “tukiendelea hivyo bila shaka hakuna chochote kitaendelea.”

Kwa muda wa miezi minne sasa naibu gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro amekuwa akiendesha kazi katika ofisi ya gavana Waititu, lakini bado inadaiwa hana mamlaka kamili ya kuteua ama kufuta mawaziri wa kaunti.

Bw Wainaina alitoa maoni hayo mnamo Jumanne mjini Thika alipokutana na wakazi wa Thika.

Vurugu

Wakati huo pia mfanyabiashara na mkazi wa Juja, Bw George Koimburi anapendekeza Kaunti ya Kiambu ivunjiliwe mbali na Rais ili uchaguzi mpya ufanywe baada ya kuwa na vurugu miongoni mwa madiwani.

“Ninapendekeza Kiambu ijipate katika hali hiyo kwa sababu ndiko Rais Uhuru Kenyatta anakotoka na kwa hivyo ili kuwe na amani inayostahili, kufanyike uchaguzi upya, ama serikali kuu iweze kuiendesha kwa muda,” alisema Bw Koimburi.

Alisema madiwani walioko katika kaunti hiyo tayari wamegawanyika kuwili na kwa hivyo hata naibu gavana Nyoro, hawezi akatekeleza wajibu wake kwa njia inayostahili.

Gavana Ferdinand Waititu bado anakabiliwa na kesi za ufisadi ambapo mahakama iliamuru akae kando huku akiendelea na kesi hiyo, naye naibu wake akachukua usukani.