Habari

Mbunge apendekeza wabakaji, wanajisi wakatwe sehemu za siri

April 12th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE Mwakilishi wa Wanawake wa Lamu katika Bunge la Kitaifa, Ruweida Obo sasa anapendekeza kuwa wanaume watakaopatikana na hatia ya kuwanajisi wasichana wenye umri mdogo waadhibiwe kwa kukatwa sehemu zao za siri.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo kwa simu Ijumaa, Aprili 12, 2019, Bi Obo amesema adhabu kama hiyo ndiyo inaafiki madhara ambayo wafanya makosa huwatendea watoto hao na kuwasababishia mfadhaiko ikiwemo unyanyapaa.

“Mshukiwa akipatikana na hatia ya kunajisi na kubaka kisha ashtakiwe na kupewa hukumu ya miaka 10 gerezani, hukumu kama hiyo haitoshani na athari ambazo wabakaji huwatendea watoto wadogo. Maisha ya mwathiriwa yataharibika kabisa,” akasema Mbunge huyo.

Akaongeza: “Hii ndiyo maana ninapendekeza ukataji wa vyungo vyao vinavyowashawishi wabakaji hao. Na kama mbunge nitawasilisha mswada bungeni kuhakikisha kuwa sheria ya kuidhinisha adhabu hiyo inaanzishwa.”

Bi Obo ni mbunge wa pili kutoa pendekezo kama hili kwa kipindi cha miezi miwili. Mnamo Februari Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Isiolo Rehema Jaldesa alitoa pendekezo hilo, akisema hiyo ndiyo njia ya kipekee ya kuzima uovu huo hasa miongoni mwa jamii za wafugaji.