Habari Mseto

Mbunge asema ni muhimu shule zitayarishwe ziweze kukabiliana na Covid-19

June 8th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MPANGO wa kuezeka shule za msingi kwa mabati ya kisasa unaleta sura mpya katika skuli hizo.

Bdhaa ya asbestos, inayodaiwa kwamba ni hatari kwa afya ya binadamu. Imedaiwa pia kuwa maji yanayotekwa kupitia kwa asbestos ni hatari kwa afya ya bianadamu.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, alisema ya kwamba baada ya kushauriana na washikadau wa elimu, waliafikiana ya kwamba ni vyema kuyaondoa mapaa hayo ili kuweka mabati ya kisasa.

“Wakati huu tunapokabiliana na Covid-19, ni vyema kuweka mikakati ifaayo kwa shule hizo za msingi ili wanafunzi wakirejea kwa masomo wapate kila kitu kipo imara,” alisema Bw Wainaina.

Alisema tayari kupitia mpango wa maendeleo wa NG-CDF afisi yake imenunua matangi ya maji 16 ya kuhifadhi lita 10,000 za maji kwa shule 16 za msingi katika eneo lake la uwakilishi.

“Nilipata ya kwamba wakati huu wanafunzi wako katika likizo kwa sababu ya Covid-19, ni vyema kuweka mikakati ya kuzuia maambukizi,” alisema mbunge huyo.

Alisema shule nyingi za msingi mjini Thika hazijawahi kufanyiwa ukarabati kwa zaidi ya miaka 20 na kwa hivyo mazingira bora katika masomo ni muhimu.

Alisema uchunguzi uliofanywa umebainisha ya kwamba mabati aina ya asbestos husababisha saratani ya mapavu na kwa hivyo kwa wakati huu hazifai kuwekwa kwenye shule.

Mbunge huyo alizuru shule kadhaa za msingi hivi majuzi na kujionea mwenyewe jinsi zinavyoendelea kufanyiwa ukarabati.

Alisema serikali inastahili kuchukua muda wake kabla ya kufungua sekta ya elimu.

“Ni vyema washikadau wote wa elimu waketi chini na kujadili jambo hilo kwa makini. Hatungetaka kushuhudia wanafunzi wakiambukizana corona kwa wingi na kusababisha taharuki nchini,” alisema Bw Wainaina.

Alisema wanafunzi watakaporejea shuleni, walimu nao wanafaa wawe na jukumu la kuwahamasisha wanafunzi jinsi ya kufuata maagizo yote ya serikali.

Mambo muhimu yanayostahili kupewa kipaumbele ni kuweka au kudumisha nafasi kutoka kwa mtu hadi mwingine, kuvalia barakoa, na kunawa mikono kila mara.

“Jambo linalostahili kuwa la lazima ni kuwa na maji mengi ya kunawa na hiyo iwe kama sheria,” alisema mbunge huyo.

Alisema kila Mkenya akifuata maagizo ya serikali bila shaka “tutaweza kurejelea shughuli zetu za hapo awali.”