Habari MsetoSiasa

Mbunge ashangaza kuwaambia waathiriwa wa mafuriko wasubiri msaada Alhamisi

December 3rd, 2019 2 min read

NA CECIL ODONGO

MBUNGE wa Nyando Jared Okello Jumanne aliwataka wakazi wa eneobunge la Nyando ambao wameathirika na mafuriko kuwa wavumilivu hadi Alhamisi ambapo ataanza rasmi kuwagawia vyakula vya msaada.

Mwanasiasa huyo alisema kwamba hana mbinu ya kusafirisha vyakula vya msaada alivyopata kutoka kwa serikali kuu na bado anajaribu kumfikia Gavana wa Kisumu Profesa Anyang’ Nyong’o ili kutafuta namna ya kufanikisha usafirishaji wa msaada huo.

“Nawaomba wakazi wa eneobunge langu wavute subira kidogo hadi Alhamisi kwa sababu kwa sasa sina namna ya kuwafikia. Hakika serikali kuu imetoa msaada wa vyakula na tunaendelea kuuhifadhi katika mji wa Awasi hadi siku hiyo tukiendelea kutafuta namna ya kuusafirisha ili ufikie wakazi,” akasema Bw Okello kwenye mahojiano na Taifa Leo.

“Kwa sasa kile ambacho tunaweza kufanya ni kuwaondoa na kuwapeleka maeneo salama na pia kuhakikisha wanapata maji safi ya kunywa ila shughuli hasa ya kusambaza vyakula itaanza Alhamisi,” akaongeza Bw Okello anayehudumu muhula wake wa kwanza.

Aidha alikiri kwamba hajapata msaada wowote kutoka kwa serikali ya kaunti ya Kisumu na alikuwa akifanya juu chini kuhakikisha anamfikia Profesa Nyong’o ili kusaidia pia kuwanusuru wakazi.

Kwa sasa wakazi walioathirika katika maeneo ya Kakola-Ombaka, Kano Kanyagwal na Nduru Kabonyo wamelazimika kukita kambi katika maeneo ya juu ya Shule ya Msingi ya Ombaka, Nyamasao na zahanati ya Kanyagwal.

Aidha mwanasiasa huyo alishukuru Shirika la Msalaba mwekundu kwa kujitolea kusaidia waathiriwa na akawaomba viongozi wote wa Nyando kuungana kuwasaidia raia.

Duru ziliarifu kwamba raia wenye hamaki walikuwa wakipanga kuandamana hadi mji wa Awasi kuvunja mahali ambapo chakula hicho kinahifadhiwa kisha kukigawa wenyewe kwa waathiriwa wa mafuriko.

Aidha baadhi ya raia wanadai mbunge huyo hajaonyesha ari ya kuwasaidia watu wa Kano kutokana na uhasama kati yake na  hasimu wake wa kiasiasa Seneta Fred Outa ambaye ana ufuasi kwenye maeneo yaliyoathirika.

Seneta huyo pia haonani uso kwa macho na Gavana Nyong’o na alikuwa mbunge wa Nyando kabla ya Bw Okello.