Mbunge ataka sheria ya kudhibiti nchi kufungwa

Mbunge ataka sheria ya kudhibiti nchi kufungwa

OSBORN MANYENGO na VALENTINE OBARA

MBUNGE wa Soy, Bw Caleb Kositany, amependekeza kuwe na sheria itakayodhibiti jinsi serikali inavyofunga sehemu za nchi, hasa wakati huu wa janga la corona.

Bw Kositany ambaye ni naibu mwenyekiti wa zamani wa chama cha Jubilee, alikosoa jinsi maagizo ya kutosafiri kutoka eneo moja hadi lingine yalivyotangazwa na Rais Uhuru Kenyatta wiki mbili zilizopita, na yakaanza kutekelezwa nchini.

Akihutubu kwenye hafla ya mazishi eneo la Matisi Kaunti ya Trans-Nzoia, Bw Kositany alisema atawasilisha mswada bungeni ili kutoa mwongozo wa utekelezaji amri za aina hiyo.

“Huwezi kutangaza lockdownsaa kumi useme inaanza usiku na kuna Wakenya wamesafiri kote nchini unawaambia wakae mahali waliko. Lazima tuwe na sheria, si watu kukaa chini na kusema funga hivi,’ akasema.

Wakati Rais Kenyatta alipotangaza kufunga kaunti tano zilizo na idadi kubwa ya maambukizi mnamo Machi 26, kuliibuka malalamishi mengi kwamba maagizo yaliyotolewa hayakutilia maanani maslahi ya wananchi.

Kwa mfano, agizo la kwamba vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zisitishe kutoa masomo ya ana kwa ana lilichukuliwa kumaanisha wanavyuo warudi nyumbani, ilhali wengine walikuwa katika kaunti zilizoagizwa zifungwe na wengine wanaoishi kaunti hizo walikuwa katika vyuo ambavyo ni vya nje.

Kando na hayo, malalamishi mengine yaliibuka kuhusu jinsi wananchi watajitafutia riziki kwani agizo hilo lilivuruga baadhi ya biashara kama vile uchukuzi.

“Zile kaunti zimefungwa huleta biashara nyingi Kenya,” akasema Bw Kositany.Kaunti zilizoagizwa kufungwa ni Nairobi, Machakos, Kiambu, Kajiado na Nakuru.Kulingana na Bw Kositany, mbinu bora zaidi ya kupambana na virusi vya corona ingekuwa kupitia kuwahimiza Wakenya kufuata sheria zote za Wizara ya Afya zinazohusu ugonjwa huo.

“Kweli tunajua kuna corona na inasambaa kwa kasi mno maeneo ambayo yamefungwa hata ingawa amri ya kutosafiri kutoka Kaunti tano haitekelezwi ipasavyo. Inafaa sheria ya afya ifuatwe na kuzingatiwa” akasema.

Mbunge wa Endebess, Dkt Robert Pukose aliwasihi Wakenya kujitokeza kwa wingi na kupokea chanjo ya kuepusha maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

Alitoa hakikisho la chanjo hiyo kuwa salama akisema kuwa yeye kama daktari amepokea chanjo hiyo na ni salama haina madhara yoyote.

Hata hivyo, aliwaonya wale ambao hunywa pombe akiwataka baada ya kupokea watulie kwa muda watakaoshauriwa na madaktari bila kunywa pombe ili dawa ipate kufanya kazi vizuri.Gavana wa Kaunti ya Trans-Nzoia, Bw Patrick Khaemba alitoa wito kwa serikali kushughulikia maswala ya maradhi mengine ikiwa ni pamoja na saratani licha ya taifa kukumbwa na janga la Covid 19.

Alitoa mfano wa ugonjwa wa saratani ambao umekuwa miongoni mwa maradhi hatari na ambayo yanaangamiza Wakenya kwa wingi.Magonjwa mengine ambayo serikali huhimizwa isisahau kukabiliana nayo ni malaria, nimonia na ukimwi.

You can share this post!

Chanjo ya AstraZeneca yaua watu saba

Mvurya ampigia debe naibu wake kuchukua usukani 2022