Habari MsetoSiasa

Mbunge ataka wasimamizi wa Nyumba Kumi wapewe bunduki

July 25th, 2019 1 min read

Na KALUME KAZUNGU

MBUNGE Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Lamu, Bi Ruweida Obbo, ameiomba serikali kuwapatia wanachama wa Nyumba Kumi bunduki ili waweze kujilinda wanapotekeleza majukumu yao mashinani.

Bi Obbo pia amependekeza serikali iwalipe wanachana hao mishahara kutokana na jukumu lao zito la kuhakikisha usalama unadhibitiwa mashinani.

Akihutubia wakazi mjini Lamu Alhamisi, Bi Obbo alisema inasikitisha kuwa wanachama wa Nyumba Kumi wamekuwa wakitelekezwa na serikali hasa kimiundomsingi licha ya kuwa kiungo muhimu katika kudhibiti usalama wa taifa.

Alisema wanastahili kupewa silaha na pia walipwe vilivyo kama njia mojawapo ya kuwapa motisha kazini.

Wanachama wengi wa Nyumba Kumi wamepoteza maisha yao wakiwa kazini kwani hulengwa zaidi na wahalifu hasa wale wa ulanguzi wa dawa za kulevya na ugaidi.

Wahalifu hao mara nyingi huwachukulia viongozi wa Nyumba Kumi kuwa maadui na pia kizingiti cha wao kuendeleza maovu yao katika jamii.

“Siridhishwi na jinsi maafisa wa Nyumba Kumi wanavyotelekezwa na serikali hasa kimiundomsingi ya kuwasaidia kutekeleza majukumu yao. Hawa viongozi wa Nyumba Kumi ndio wa kwanza kufuatwa na wahalifu ambao mara nyingi huwatishia maisha na hata kuwaua mashinani. Ni vyema wapewe bunduki ili kujilinda kazini. Isitoshe, serikali iwazingatie maafisa hao kwa kuwapa mishahara,” akasema Bi Obbo.

Alitoa mfano wa chifu aliyevamiwa na kuuawa na wahalifu mchana eneo la Mbwajumwali, Kaunti ya Lamu kuwa tukio linalofaa kuisukuma serikali kuwapa maafisa wa Nyumba Kumi bunduki.

“Najua kuna mjadala kuhusu machifu kupewa bunduki. Tayari kumekuwa na mafunzo maalum ya kiusalama kwa machifu hao kote nchini. Ikiwa chifu anaweza kuvamiwa na kuuawa mchana siku ya Ramadhani eneo hili, sembuse afisa wa Nyumba Kumi ambaye hana silaha yoyote?” aliuliza.

Aliongeza, “Nyumba Kumi wapewe silaha ili kuwahimiza kutekeleza majukumu yao kwa ukamilifu zaidi.”

Wakati huo huo, alihimiza serikali kuzingatia angalau uwepo wa thuluthi mbili za kila jinsia inapoajiri maafisa wa usalama kote nchini.