Habari

Mbunge atoa mayai 10,800 kwa watahiniwa wa KCPE ili 'kuboresha matokeo'

October 26th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

MBUNGE wa Thika Patrick Wainaina ametoa zawadi ya kipekee kwa wanafunzi 3,600 wanaofanya mtihani wa kitaifa wa KCPE mwaka huu, baada ya kuwanunulia yai kila siku, kwa siku tatu watakazofanya mtihani huo.

Kulingana na mbunge huyo, ulaji wa mayai yake utawasaidia wanafunzi kupata motisha na kuzidisha umakinifu wakati watakapokuwa wakifanya mtihani huo unaoanza Oktoa 30. Mbunge huyo atatoa jumla ya mayai 10,800 katika siku hizo.

Akizungumza katika afisi za CDF za Thika Ijumaa, mbunge huyo alieleza kuwa zoezi hilo litasaidia kurekebisha hali ya matokeo mabaya ya KCPE ambayo yamekuwa yakishuhudiwa eneobunge hilo.

“Hii ni hatua ndogo lakini tunatarajia kuwa itasaidia kurekebisha hali na kuwapa motisha wanafunzi ili wahitimu vyema,” akasema.

Aidha, aliahidi kuwatuza wanafunzi wote watatu bora katika kila shule ya eneobunge lake, wa kuanzia darasa la kwanza had inane.

Zoezi hilo alisema ni la kupiga jeki lile la “Jumatatu ya yai” (egg Monday) lililoanzishwa Mei, ambapo wanafunzi wote wa shule za umma wamekuwa wakipokea yai kila Jumatatu, akisema zoezi hilo limesaidia idadi ya wanafunzi wanaohudhuria masomo kuongezeka.

“Hata baadhi ya wanafunzi wamehama kutoka shule za kibinafsi kuja za umma kutokana na zoezi hilo la kuwapa mayai,” akasema.