Michezo

Mbunge azindua mashindano ya michezo Gatundu Kaskazini

August 22nd, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Gatundu Kaskazini, watafurahia kushuhudia michezo ya vijana ya Sports Talent League kwa muda wa miezi mitatu mfululizo.

Mashindano hayo yanashirikisha timu za soka ya vijana wa kiume zipatazo 48 na nane za wasichana.

Inashirikisha pia michezo ya vishale na voliboli kwa walemavu.

Mashindano hayo yanadhaminiwa na Mbunge wa eneo la Gatundu Kaskazini Anne Wanjiku Kibe ambaye amesema atahakikisha vijana wanaonyesha talanta zao ili waweze kujiuza siku za usoni.

Mashindano hayo yalizinduliwa rasmi mnamo mwishoni mwa wiki jana huku yakihudhuriwa na mashabiki wengi ajabu katika uwanja wa Nyamathumbi, Gatundu Kaskazini.

Kulinagana na mpangilio wa mashindano hayo, katika michezo ya soka kwa wavulana mshindi atapokea kitita cha Sh70,000.

Mshindi wa pili atapokea Sh50,000 na timu itakayoibuka ya tatu itapokea Sh30,000. Watakaomaliza nambari nne wataridhika na Sh10,000.

Katika kiwango cha walemavu mshindi atapokea Sh20,000. Wa pili 15,000 naye mshindi wa tatu ataridhika na Sh10,000 huku wa nne akiburudika na Sh5,000.

Alisema mpango huo wa kuzindua michezo eneo lake ni muhimu kwa sababu utapunguza uhuni na hali ya usalama itaimarika.

“Nina hakika kila kijana ataona umuhimu wa kujihusisha na michezo hasa spoti ili kuwa mwananchi mwema wa kutegemewa siku zijazo ,” alisema Kibe.

Alisema tayari amepata habari kuhusu upungufu wa marefarii katika sekta ya mchezo wa soka na kwa hivyo, atafanya juhudi kuona ya kwamba wengi wanapata mafunzo kupitia Shirikisho la Soka nchini FKF ili wainue hali ya michezo mitaani.

“Mimi kama kiongozi anayedhamini michezo nitahakikisha ninatoa fedha zangu kuona ya kwamba nimeboresha michezo kwa jumla katika Gatundu Kaskazini na maeneo ya karibu.

Mbunge huyo ni mmoja wa wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Michezo na ndiyo maana amechukua jukumu la kuinua kiwango cha michezo eneo lake.

Vijana wahimizwa kutia bidii

Aliwahimiza vijana wajitokeze kwa wingi na kufanya mazoezi kwa bidii ili kuimarisha afya zao na kushiriki michezo mbalimbali.

Aliongeza kwamba ananuia kujenga kituo cha wanamichezo ambacho kitakuwa na vifaa vyote muhimu.

Aliongeza mpango huo ukifanikiwa bila shaka kutapatikana wanamichezo wengi wa kutegemewa kutoka huko.

Alisema pia kutakuwa na chuo cha kiufundi ili vijana wengi walio mashinani waweze kupata mafunzo ya kujitegemea kando na kuwa wanaspoti hodari.

Wakati wa uzinduzi huo mechi kadha zilichezwa za akina dada na vilevile za wavulana.

Timu ya Kiangunu Ladies iliichabanga Chania Ladies mabao 5-3 kupitia mikwaju ya penalti.

Halafu timu ya wavulana ya Gatei FC iliikomoa Kariua FC kwa mabao 2-0.

Nayo Kiriko FC iliipiga Nyamathumbi FC mabao 2-0.

Mashindano hayo yataendelea kila wiki katika uwanja wa Nyamathumbi, Gatundu Kaslazini.