Habari Mseto

Mbunge Gabriel Kagombe kuendelea kuwa mgeni wa polisi

June 4th, 2024 1 min read

NA PIUS MAUNDU

MBUNGE wa Gatundu Kusini Bw Gabriel Kagombe ataendelea kuzuiliwa na maafisa wa polisi hadi Ijumaa atakaposomewa mashtaka.

Hii ni baada ya mahakama kuu ya Machakos kufutilia mbali ombi lake la kuachiliwa kwa dhamana.

Bw Kagombe alitiwa kizimbani baada ya kukamatwa kwa madai ya mauaji ya mhudumu wa boda boda Bw David Nduati Wataha.

Alipofikishwa mahakamani hapo jana, Bw Kagombe hakuitika mashtaka badala yake hakimu mkuu wa mahakama hiyo alitoa agizo la kufanyiwa uchunguzi wa akili.

“Kabla ya kusomewa mashtaka, mshukiwa apelekwe hospitali ya rufaa ya kaunti ya Kiambu ili kubaini kama yuko na akili timamu kujibu mashtaka,” alisema hakimu Francis Rayola.

“Kuhusu iwapo mshtakiwa anafaa kuachiliwa kwa dhamana na kuangalia maelezo yaliyotolewa katika mahakama kuu ya Kiambu kuhusuina na swala la kuachiliwa kwa dhamana, mshukiwa atatakiwa kufanya upya ombi la kupewa dhamana baada ya kusomewa mashtaka,” alisema Jaji Rayola.

Mikosi ilimkumba mbunge huyo wa awamu ya kwanza alipoandamana na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa na Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwah, Mbunge wa Gatundu Kaskazini Elija Njoroge, Mbunge wa Thika Mjini Alice Ng’ang’a na wanasiasa wengine wa Kiambu wakati wa uzinduzi wa soko wiki mbili zilizopita.

Mbunge huyo, anadaiwa kufyatua risasi wakati makundi mawili ya wanasiasa wa Kiambu na wafuasi wao walipokabiliana kuhusu mradi wa soko uliopendekezwa.

Kulingana na stakabadhi ya mashtaka iliyowasilishwa kortini, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma anapanga kumfungulia mashtaka mbunge huyo ya kumuua Bw Nduati.

“Mnamo tarehe 17 Mei, 2024, mwendo wa saa kumi na nusu jioni katika eneo la Kimuchu eneo la Makongeni katika Kaunti Ndogo ya Thika Magharibi ndani ya Kaunti ya Kiambu alimuua David Nduati Wataha,” stakabadhi hiyo ilisoma.

Stakabadhi hiyo ya mashtaka ilitiwa saini na, Mkurugenzi msaidizi wa Mashtaka kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mashtaka Bw Gikuhi Gichuhi.