Mbunge Hassan aomba baraza la kiswahili kubuniwa nchini

Mbunge Hassan aomba baraza la kiswahili kubuniwa nchini

Na WANGU KANURI

Mbunge wa Kamukunji, Yusuf Hassan ameitaka serikali kuu kupitia Wizara ya Michezo, Utamaduni na Urithi kuanzisha rasmi Baraza la Kiswahili la Kitaifa.

Isitoshe, wizara hiyo inapaswa kuhakikisha kuwa vyombo vya kitaifa na vya kibinafsi vinavyohusika na uboreshaji wa lugha ya Kiswahili vimeshirikiana katika uundaji wa baraza hilo. Akirejelea pendekezo la 2018 ambalo liliidhinisha kubuniwa kwa baraza la Kiswahili na Baraza la Mawaziri la nchi hiyo, Bw Hassan alisema kuwa kubuniwa kwa baraza hilo kutasaidia kuimarisha lugha ya Kiswahili.

“Lugha ya Kiingereza ina nguvu sana katika mawasiliano rasmi na kwa hivyo inachangia katika kudhoofisha lugha yetu ya Kiswahili,”akasema. Katika ombi la 2018, baraza hilo lililokuwa libuniwe, lilipaswa kutoa ushauri, kuimarisha uongozi wa serikali kuhusiana na ukuzi, ulinzi na pia kuunga mkono matumizi ya lugha ya Kiswahili.

Isitoshe, ukuzi na utumiaji wa lugha ya Kiswahili kama lugha ya Jumuiya ungeimarishwa kama ilivyodondoshwa kwenye kipengee 137 cha Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika Katiba ya Kenya, Kiswahili kimebainishwa kama lugha ya Kitaifa na pia lugha rasmi.

Kiswahili ni lugha ya kiasili haswa kwa jamii za mkoani wa pwani nchini Kenya na pia kuna idadi kubwa ya Wakenya wanaozungumza lugha hiyo. “Serikali imepewa wajibu wa kulinda na kuendeleza lugha tofauti za watu wa Kenya na kukuza matumizi ya lugha za kiasili nchini,” akasema.

Hata hivyo, Bw Hassan alieleza kuwa itakuwa vyema Kenya ikiwa na baraza lake kama nchi ya Tanzania na visiwa vya Zanzibari. Mnamo mwaka wa 1967, Tanzania iliunda Baraza la Kiswahili la Kitaifa (BAKITA) nayo Zanzibari ikibuni Baraza la Kiswahili la Zanzibari (BAKIZA) mnamo mwaka wa 2004.

You can share this post!

Leicester inafaa kujilaumu kubanduliwa Ligi ya Uropa

Matano roho juu CS Sfaxien ikiwasili, Gor ziarani Congo

T L