Habari za Kitaifa

Mbunge huru baada ya siku tatu rumande

June 7th, 2024 1 min read

NA PIUS MAUNDU

MBUNGE wa Gatundu Kusini, Gabriel Kagombe, amepata afueni baada ya Mahakama ya Machakos kumuachilia kwa dhamana ya Sh2 milioni au pesa taslimu Sh1 milioni, katika kesi anayodaiwa kumuua mhudumu wa bodaboda mjini Thika, Kaunti ya Kiambu.

Mbunge huyo amekuwa rumande kwa siku tatu zilizopita kuhusiana na mauaji ya Bw David Nduati Wataha mnamo Mei 17, 2024. Alikana mashtaka alipofika mbele ya Jaji Francis Rayola.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma alitaka Bw Kagombe azuiwe kuingia katika mji wa Thika, akidai kuwa ana ushawishi mkubwa na anaweza kuingilia mashahidi.

Mawakili wa familia ya mwathiriwa walitaka mbunge huyo kuzuiwa kufika na kufanya mikutano katika katika Kaunti ya Kiambu.

Bw Rayola alimzuia mbunge huyo kuzuru eneo la Kimuchu, Kaunti Ndogo ya Thika Magharibi, Kaunti ya Kiambu ambapo kisa hicho kilitokea.

Siku anayodaiwa kutekeleza mauaji hayo, mbunge huyo alikuwa ameandamana na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa na Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwah, Mbunge wa Gatundu Kaskazini Elija Njoroge, Mbunge wa Thika Mjini Alice Ng’ang’a na wanasiasa wengine wa Kiambu

Alidaiwa kufyatua risasi wakati makundi mawili ya wanasiasa na wafuasi wao yalipokabiliana. Kesi itatajwa Julai 17, 2024.