Habari

Mbunge Ken Okoth wa Kibra afariki

July 26th, 2019 1 min read

Na MWANDISHI WETU

MBUNGE wa Kibra, Ken Okoth amefariki katika Nairobi Hospital ambako alikuwa amepelekwa kupokea matibabu akiwa katika hali mbaya kiafya.

Alikuwa akiugua maradhi ya saratani ya utumbo na jana Alhamisi.

Mzawa wa mwaka 1978, mbunge huyo ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 41.

Okoth atakumbukwa kwa weledi wake hasa ulumbi na vilevile mkakati wa kuongoza eneobunge lake kwa msingi wa rekodi bora ya maendeleo.

Ni takribani kipindi cha wiki mbili tu zilizopita ambapo mbunge huyo alikuwa amerejea nyumbani kutoka Ufaransa ambako alikuwa akipokea matibabu kwa miezi mitano.

Mara aliporejea nchini mbunge huyo alihuduria Tamasha za Muziki za Kibra Music Festival katika Shule ya Moi Girls, Nairobi, alipoimba maneno machache ya wimbo “Roho Yangu” utunzi wake msanii Rich Mavoko.

“Hayo maneno walinena wazee wa zamani,; ukiwa mjanja kuchapiwa ni siri ya ndani,” aliimba Okoth wakati huo.

Kimsingi ubeti huo unamaanisha kuwa ni jambo la hekima kusikiza mawaidha ya wazee.

Alitumia fursa hiyuo kumshukuru mwenzake wa Westlands Tim Wanyonyi ambaye alikuwa akisambaza hundi za basari kwa shule katika eneobunge hilo kwa niaba yake (Okoth).