Habari

Mbunge Kimani Ngunjiri apokonywa bunduki

January 21st, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Bahati, Kimani Ngunjiri amewasilisha bunduki yake kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Jumanne baada ya serikali kufutilia mbali leseni yake ya kumiliki silaha hiyo.

Walinzi wa mbunge huyo mbishani pia wameondolewa, amedai.

Hatua hiyo yumkini inatokana na usemi wake mwishoni mwa wiki ambapo alidai serikali inamhangaisha Naibu Rais William Ruto kwa kumzuia kutumia makazi yake rasmi mjini Mombasa.

Ilidaiwa kuwa matamshi kama haya yanaweza kuchochea fujo na uhasama katika eneo la Rift Valley.

Bw Ngunjiri, ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto na mwanachama wa mrengo wa ‘Tangatanga’, alisema kuwa hatabadili msimamo wake wa kumpigia debe Dkt Ruto.

Mbunge huyo aliamriwa kurejesha bunduki yake baada ya kudadisiwa na maafisa wa DCI mjini Nakuru.

Akiongea na wanahabari baadaye, Bw Ngunjiri amesema alitakiwa kuthibitisha madai yake.

“Nashangaa ni kwa nini wananiuliza nifafanue madai yangu, ilhali habari hizo zilichapishwa magazetini hivi majuzi. Wanafaa kuwauliwa wanahabari ambao walichapisha habari hizo,” akasema.

Bw Ngunjiri amesema malalamishi yake yalikuwa kwamba Dkt Ruto alifurushwa kutoka makazi yake rasmi na kwamba hakunuia kuchochea uhasama na fujo.