Habari MsetoSiasa

Mbunge kituoni baada ya kuzaba mkazi makofi

June 5th, 2019 1 min read

NA MWANDISHI WETU

MBUNGE wa Gem, Elisha Odhiambo ameandikisha taarifa kwa polisi kufuatia kisa ambapo alidaiwa kumshambulia mwanamume mjini Kisumu mnamo Jumanne alasiri.

Katika video ya sekunde 41 inayosambaa mitandaoni, mbunge huyo anaonekana akimkabili Maurice Ochieng’ Oduor katika eneo la Biashara Market, na kumzaba makofi akidai jamaa huyo aliweka ujumbe katika facebook kwamba mbunge huyo alikuwa amekamatwa na maafisa wa EACC awali siku hiyo.

Bw Odhiambo alikuwa ameandamana na wasaidizi wake ambao Bw Oduor alidai pia walimpiga kabla ya kuondoka.

Mbunge huyo ameagizwa kupiga ripoti katika afisi za Idara ya Upelelezi wa Jinai mjini Kisumu hapo Juni 17.

“Niliweka matukio katika ukurasa wangu wa facebook nikiwaarifu marafiki zangu kuhusu yale yanayotendeka Kisumu. Hapo ndipo nikaanza kupokea simu nyingi kutoka kwa wafuasi wa mheshimiwa wakiuliza kwa nini naharibu jina la mbunge huyo,” akasema Bw Oduor.

Alisema baadaye aliondoa ujumbe huo na akaamua kumpigia simu Bw Odhiambo na wawili hao wakakubaliana kukutana na hapo ndipo alipopigwa.