Habari MsetoSiasa

Mbunge maalum ataka Munya ajiuzulu

August 12th, 2019 1 min read

Na DAVID MUCHUI

MBUNGE maalum, Bi Halima Mucheke amemtaka Waziri wa Biashara Peter Munya ajiuzulu kwa kuruhusu kuuzwa kwa mafuta yasiyofaa kuliwa na binadamu.

Akizugumza katika shule ya Sekondari ya Gikumene iliyoko kaunti ya Meru Jumapili alipoandamana na naibu wa Rais William Ruto kuchangisha harambee, Bi Mucheke alisema hakuna mtu anayepasa kuachwa katika vita dhidi ya ufisadi.

“Sitanyamaza huku Wakenya wakipewa chakula duni eti kwa sababu kuna baadhi ya watu wanaopendelewa licha ya kuhusika na ufisadi. Sitaogopa kusema kwa sababu niliteuliwa kutetea haki. Ikiwa umeruhusu kuuzwa kwa mafuta yasiyofaa basi wapasa kujiuzulu,” Bi Mucheke alisema.

Matamshi hayo yamefuatia ripoti kwamba mkurugenzi wa uchanguzi wa jinai (DCI) alifichwa uamuzi wa kuachiliwa kwa mafuta hayo yaliyobanwa mwaka uliopita ukichukuliwa.

Mafuta hayo yalikamatwa na kuzuiliwa na maafisa wa ukadiriaji wa ubora wa bidhaa kwa vile hayakuwa na virutubishi vya Vitamini A.

“Ikiwa DCI anatekeleza kazi yake ipasavyo basi inambidi ahakikishe CS muhusika amejiuzulu uchunguzi ufanywe,” alisema.

Bi Mucheke,aliyekashfiwa kwa matamshi hayo aliwaeleza wapinzani wake hatatishika kwa vile suala hilo linahusu maslahi ya umma.

DCI anamchunguza Bw Munya kwa kuamuru mafuta hayo yaachiliwe bila masharti.