Habari za Kitaifa

Mbunge, Maimam wazozania chakula cha msaada

March 18th, 2024 2 min read

NA WINNIE ATIENO

UGAVI wa chakula cha msaada kwa jamii ya Waislamu umegeuka kuwa wa kisiasa baada ya Mbunge wa Nyali, Bw Mohammed Ali na viongozi wa kidini wakiongozwa na Baraza Kuu la Kiislamu (SUPKEM) na wenzao la Maimamu wa Kiislamu Kenya (CIPK) kuanza kulumbana kuhusu zoezi hilo.

Utata huu ulianza pale serikali ya Kenya Kwanza ilipobadilisha desturi ya ugavi wa chakula kutoka kwa viongozi wa kidini na kuukabidhi wanasiasa.

Viongozi wa mabaraza hayo mawili walilalamikia hatua hiyo wakiuliza sababu za serikali kuwapa wanasiasa jukumu la kugawa vyakula wakati wa Ramadhan kwa waislamu wanaoendelea na mfungo wao.

Viongozi hao wa kidini wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Waislamu nchini, Athman Akbar walisema kwa miaka mingi imekuwa ni desturi kwa serikali kuwakabidhi jukumu hilo la kusambaza vyakula vya msaada kwa wasiojiweza.

Hata hivyo, walishangaa kumwona Bw Ali akiendeleza zoezi hilo mitaani na kuikashifu hatua hiyo.

Bw Akbar alisema kila mwaka, inapofika Mwezi wa Ramadhani, Serikali Kuu hupeana msaada wa chakula kupitia SUPKEM na CIPK kukisambaza katika kaunti zote nchini.

Bw Akbar alisema mashirika hayo mawili ya Kiislamu hukabidhiwa mamlaka kugawa chakula cha msaada ili yasambaze kwa sababu yana idadi ya misikiti, madrasa na makao ya mayatima.

“Kama desturi kila mwaka huwa tunaandika barua kwa kamishna wa kaunti na baadaye huwa tunapewa barua kwamba tutaletewa chakula tarehe fulani. Ni mwaka wa saba sasa tumekuwa tukipewa chakula kusambazia Waislamu,” alisema Bw Akbar.

Hata hivyo, mwaka huu walishangaa baada ya serikali ya Kenya Kwanza kuchukua mkondo mpya.

“Tulipoenda kwa kamishna wa kaunti, alituambia kuwa amepata maagizo kutoka kwa Waziri kwamba chakula kitapewa Mbunge wa Nyali na Seneta Mteule Bi Miraj Abdhallah. Wao ndio walitajwa kusimamia ugavi wa chakula cha Waislamu,” alisema Bw Akbar.

Alisema viongozi wa kidini hawangelalamika endapo wabunge wote wa Mombasa wangehusishwa kwenye zoezi hilo.

“Lakini kwa nini wamechukua mrengo mmoja wa kisiasa?” aliuliza kiongozi huyo wa kidini.

Viongozi wa CIPK nao walisema ni makosa kwa serikali kupeana chakula hicho kwa wanasiasa badala ya viongozi wa kidini kama desturi.

Hata hivyo, kwa upande wake Bw Ali aliwashtumu viongozi hao wa kidini akisema chakula hicho kinaweza kusambazwa na Muislamu yeyote.

Bw Ali alisema alitwikwa jukumu hilo na Rais William Ruto na wala hakujituma.

“Nimesikia hizo kelele mnapiga, tulizeni boli, fanyeni kazi inayowahusu. Fanyeni masuala ya kidini, kutusaidia tupigane na wezi, dawa za kulevya, ufisadi lakini chakula itafika kwa maskini mpende msipende,” alisema Bw Ali.

Akiongea kwenye zoezi la ugavi wa chakula katika mitaa duni ya Moroto, Kaa Chonjo, Maguniani na Burukenge, Mbunge Ali alisema chakula hicho ni cha serikali kuu.

“Kwa hivyo mimi nimeambiwa kama kiongozi wa UDA, mbunge wa kipekee niweze kuleta hiki chakula hapa na ndio maana nimekileta. Mlikuwa mwataka nipeane mletewe? Itafika? Mshawahi kupewa?” aliuliza wakazi hao.

Mbunge huyo alisema kwa zaidi ya miaka 20 ambayo jukumu hilo lilikuwa limekabidhiwa viongozi hao wa kidini, kuna Waislamu wengi walikuwa hawasambaziwi chakula.

Aliwataka viongozi hao wa SUPKEM kumheshimu na kushughulikia masuala yanayowahusu.