Habari

Mbunge motoni kumkemea Rais

January 4th, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

MBUNGE wa Kandara, Bi Alice Wahome amejipata matatani kwa matamshi yake ambayo wandani wa Rais Uhuru Kenyatta wanayachukulia kama ya kumdhalilisha Rais.

Viongozi waliojumuisha Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyikazi (Cotu), Bw Francis Atwoli, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Murang’a, Bi Sabina Chege na aliyekuwa Gavana wa Kiambu, Bw William Kabogo, walimshutumu mbunge huyo kwa kuendeleza ‘siasa za pesa nane’ badala ya kushughulikia matatizo ya watu waliomchagua.

Bw Atwoli aliyataja matamshi ya Bi Wahome kama tisho kwa demokrasia nchini.

“Kila Mkenya ana haki ya kuwania wadhifa wowote anaotaka. Nashangaa kwamba Bi Wahome, baada ya kumlilia Rais Uhuru Kenyatta ahakikishe demokrasia na masuala yanayohusiana na Katiba yanaheshimiwa, sasa amebadili msimamo,” akasema.

Akizungumza mjini Nakuru, Bw Atwoli alisitiza kuwa mwito wa kuwa na serikali inayojumuisha wote utaendelea kwa ajili ya umoja na amani nchini.

“Kila Mkenya ana haki ya kuwania wadhifa anaotaka. Wakati umewadia wa sisi kuangalia katiba mpya….tuyatambue mapungufu katika hii katiba. Moja ni mambo ya uongozi…mtu mmoja akipata urais anachukua viti vyote na anawacha wengine nje. Ni lazima watu wakimaliza uchaguzi, vile vyama vikubwa ambavyo vimepata wabunge wengi vishirikishwe katika serikali. Hiyo italeta amani. Huyo Alice asiseme huu ndio uhuru wa kuongea anaotaka,” akasema.

Bi Wahome akizungumza mjini Malindi Alhamisi alidai Rais Kenyatta ndiye tisho kuu kwa nchi katika masuala ya uchumi, demokrasia na uhuru wa kuzungumza.

Kulingana na mbunge huyo, Rais Kenyatta alirithi demokrasia thabiti kutoka kwa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, lakini hali imedorora.

Alidai kuwa Rais Kenytta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, wana njama ya kutumia ripoti ya BBI kama mamluki wa kisiasa bila kujali Katiba, ili wakwamilie mamlakani baada ya mwaka 2022.

Lakini Bi Chege alimtaka Bi Wahome anayetoka naye kaunti ya Murang’a ashughulikie vyoo vilivyo katika hali mbaya Kandara ambako wakazi wako nyuma kimaendeleo.

Akizungumza Ijumaa mjini Kenol alipotoa hundi za ufadhili wa masomo kwa watoto werevu kutoka familia maskini, Bi Chege alimkemea Bi Wahome na wabunge wote wa mrengo wa ‘Tangatanga’ kwa kutumia jina la Rais Kenyatta kuendeleza siasa duni.

“Huu ni upumbavu wa hali ya juu kwa mbungekutoa taarifa kwenye mahoteli na kusahau kuwafanyia kazi waliomchagua. Watu wa Kandara wanateseka. Vyoo viko katika hali duni. Yeye kila siku ni kusafiri kwa ndege na Naibu Rais William Ruto ambaye hawamuulizi chochote kuhusu uchumi mbaya. Daima wao kazi yao ni kumkashifu Rais,” akasema.

Alidai Bi Wahome ana uchungu kwa kuwa mpango wa kuwazoma waombolezaji wakati wa mazishi wa mwanasiasa Charlea Rubia haukufaulu.

Kwa upande wake, Bw Kabogo alimshutumu Bi Wahome kwa kutumiwa na baadhi ya watu ndani ya Jubilee walio na maono ya urais kumdharau na kumpiga vita Rais Kenyatta, ili aonekane kiongozi ambaye jamii iliyompigia kura kwa wingi haimtaki tena.

“Kama Alice Wahome anaamini Ruto anaweza kufanya vyema zaidi ni kwa nini ameshindwa kuzuia ufisadi nchini, ikizingatiwa kuwa alichaguliwa kwa tikiti moja na rais Kenyatta?” akauliza alipozungumza na Taifa Leo kwa njia ya simu. Mbunge wa Nyeri mjini Ngunjiri Wambugu alisema Bi Wahome anateta kwa sababu amelipwa. “Watu wakule pesa walizolipwa pole pole,” aliandika kwenye Twitter. Naye mbunge wa Tiaty William Kamket alimtaka Bi Wahome kukoma kumshambulia rais. “Achana na Rais na ushughulikie matatizo yako peke yako,” alisema.

Mkurugenzi wa mawasiliano wa chama cha ODM Philip Etale pia alimtaka Bi Wahome kukoma kumdunisha Rais. Mwakilishi wa wanawake kaunti ya Busia Florence Mutua alimtaka Bi Wahome kutohusisha viongozi wengine na masaibu yake.

 

Ripoti za NDUNGU GACHANE, SIMON CIURI na MERCY KOSKEI