Habari Mseto

Mbunge na mlinzi wake kufunguliwa mashtaka

May 14th, 2018 1 min read

Na MAGATI OBEBO

MBUNGE wa Bobasi Innocent Obiri na mlinzi wake wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo mjini Kisii ambapo watafunguliwa mashtaka ya uchochezi na kuzua vurugu.

Bw Obiri alinaswa karibu na hoteli ya Hilton jijini Nairobi mnamo Jumamosi, naye mlinzi wake akatiwa mbarobi katika eneo la Kitengela, Kaunti ya Kajiado.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kisii Abdi Hassan alisema Bw Obiri atafunguliwa mashtaka ya uchochezi, kuzua vurugu, uharibifu wa mali atakapofikishwa mahakamani leo.

“Tumekamilisha uchunguzi hivyo wawili hao watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka hayo,” akasema.

Wawili hao walinaswa kuhusiana na kisa cha wiki iliyopita ambapo walienda katika timbo la kibinafsi katika eneo la Masongo, Nyamonema Bobasi na kuwashambulia wafanyakazi kutokana na madai kuwa mlio wa kupasua mawe timboni ulipigia kelele wakazi.