Michezo

Mbunge ndani kwa kumzaba kofi kamanda wa polisi

May 19th, 2019 1 min read

Na FRANCIS MUREITHI

MBUNGE wa Nakuru Town Mashariki David Gikaria alikamatwa Jumamosi kwa kumzaba kofi kamanda wa polisi na kusababisha fujo katika mtaa wa Pipeline, Kaunti ya Nakuru.

Polisi walimkamata Gikaria kwa kuhusika katika fujo hizo za ardhi inayosemekana kumilikiwa na meya wa zamani wa Nakuru.

Naibu Kamanda wa Polisi, Kaunti ya Nakuru, Bw Kirinya Limbitu, alisema kuwa mbunge huyo pia atakabiliwa na mashtaka ya shambulio baada ya kumpiga kofi naibu kamanda wa polisi wa kaunti ndogo.

Bw Limbitu alisema mbunge huyo mtatanishi anazuiliwa katika kituo cha polisi ambacho hakukitaja, na atafikishwa mahakamani Jumatatu.

Kulingana na duru za polisi mashinani, mbunge huyo anasemakana kujiunga na kundi la vijana waliokuwa wakijenga vifaa haramu katika sehemu ya shamba hilo la ekari tatu linalomilikiwa na meya wa zamani Mohammed Surraw.

Vijana kadhaa waliopatikana shambani humo walikamatwa huku vifaa vya ujenzi pamoja na pikipiki vikinaswa na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Nakuru Central. Kwa wakati mmoja, polisi walilazimika kufyatua gesi ya kutoa machozi hewani ili kutawanya vijana hao ambao pia walifunga barabara kuu ya Nakuru-Nairobi wakitumia miti na mawe.

“Tulipokea habari kwamba Bw Gikaria na diwani wa hapo Humphrey Mwaniki walikuwa wakipanga kuongoza vijana kadhaa kujenga vifaa kwenye ardhi ya kibinafsi, tukachukua hatua na kutawanya vijana hao,” alieleza Bw Limbitu.

Kamanda huyo wa polisi aliambia Taifa Jumapili kwamba utata wa umiliki unaozingira shamba hilo bado ni suala linaloshughulikiwa kortini. Vilevile, alidai kuwa mbunge huyo wa Nakuru Town Mashariki alimshambulia kamanda wa polisi wa kaunti-ndogo wakati wa fujo hizo.

“Ni kweli kwamba alimpiga mmoja wa maafisa wa polisi wa ngazi ya kamanda wa polisi wa kaunti ndogo, na tutamfungulia mashtaka ya shambulio,” akasema Bw Limbitu.

Bw Surraw alidai kuwa viongozi hao wawili wanamezea mate shamba lake na wanapanga kulinyakua.