Habari za Kitaifa

Mbunge wa Amerika akemea IMF kwa kusababisha Serikali ya Kenya kuleta ushuru wa juu

Na LABAAN SHABAAN June 27th, 2024 1 min read

MBUNGE wa Amerika Ilhan Omar amelaumu Hazina ya Fedha ya Kimataifa (IMF) kwa misururu ya ushuru iliyolimbikiziwa Wakenya katika Mswada tata wa Fedha wa 2024 unaopingwa na wananchi hasaa vijana wa kizazi cha Gen Z.

“Ni muhimu kutambua kuwa masharti makali ya kifedha ya IMF yamechangia hali ngumu ya kiuchumi inayowakumba wananchi wa Kenya. Mikakati hii aghalabu huathiri vibaya watu wasiojiweza na inaweza kuzidisha matukio ya  maandamano ya wananchi dhidi ya serikali,” ilisema taarifa ya Mbunge Omar iliyopackiwa katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X.

Kwa moto uo huo, Mjumbe huyo wa Wilaya ya Tano ya Minnesota (Minnesota’s 5th District) amekemea serikali kwa maafa ya waandamanaji na uharibifu unaoshuhudiwa nchini katika kipindi ambacho Wakenya wanapinga sera dhalimu ya utozaji ushuru.

“Ripoti ya polisi kutumia nguvu nyingi na risasi, wakilenga wanahabari, na kuteka nyara waandamanaji, zinasikitisha na lazima ziangaziwe,” alisema Bi Omar.

“Serikali ya Kenya lazima ifichue walipo waandamanaji na hali zao baada ya kukamatwa ama kutoweka.”

Mbunge huyo kadhalika ametaka serikali kusikiza kilio cha Wakenya kupitia utaratibu wa mazungumzo yanayoweza kuzaa matunda.

Wakenya wanaojihusisha na maandamano yanayoendelea wametakiwa kudumisha amani huku serikali ikihitajiwa kuheshimu haki zao za kikatiba wanapokosoa serikali kwa njia hii.