Habari Mseto

Mbunge wa Kenya Kwanza aapa kupinga Mswada wa Fedha


MBUNGE wa mrengo wa Kenya Kwanza katika Kaunti ya Kwale, ameapa kupinga Mswada wa Fedha unaopangwa kujadiliwa wiki hii.

Mbunge wa Lunga Lunga, Bw Mangale Chiforomodo, ambaye ni mwanachama wa UDM kilicho kwenye mrengo wa Kenya Kwanza, amesema baadhi ya mapendekezo ambayo yataumiza Wakenya katika mswada huo lazima yakataliwe.

Bw Chiforomodo alisema hatashurutishwa na yeyote kuunga mkono mswada huo licha ya kuwa kwenye mrengo wa Kenya Kwanza.

“Wabunge si watoto. Tutafanya kazi zetu kwa mujibu wa sheria,” alisema mbunge huyo.

Wakati huo huo, viongozi wa Kwale wamewasihi wakazi kujiunga na vyama vya ushirika ili kuchukua mikopo ya kujiendeleza kibiashara.

Wakiongozwa na Naibu Gavana, Bw Chirema Kombo, walisisitizia umuhimu wa wakazi kuwa na elimu kuhusu fedha.

Walikuwa wakiongea kwenye uzinduzi wa chama cha ushirika cha Tuchape Kazi Sacco eneo la Lunga Lunga mjini.