Habari za Kitaifa

Mbunge wa Kenya Kwanza apinga pendekezo la kupandisha bei ya mkate

March 15th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Mukurwe-ini John Kaguchia kwa mara ya kwanza amepinga sera ya serikali ya Kenya Kwanza inayolenga kuiongezea mapato.

Bw Kaguchia ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA), anapinga pendekezo la Wizara ya Fedha kuanzisha ushuru wa ziada ya thamani (VAT) kwa mkate na maziwa.

Kwenye mahojiano, mbunge huyo anayehudumu muhula wa kwanza aliwataka wabunge wenzake kupinga pendekezo hilo kwa sababu litachangia kuongezeka kwa gharama ya maisha.

“Ingawa serikali inatafuta njia za kuongeza mapato, haifai kufanya hivyo kwa kuanzisha ushuru zaidi kwa bidhaa za kimsingi kama vile mkate na maziwa. Hatua kama hii itaongeza gharama ya maisha. Hatuwezi kuunga mkono pendekezo kama hili,” Bw Kaguchia akasema Alhamisi asubuhi kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen.

Mbunge huyo alisema bunge litatoa mwelekeo kwa Wizara ya Fedha kuhusu bidhaa ambazo zinafaa kutozwa ushuru wa juu na zile ambazo hazistahili kuguswa “kwani zaweza kuwaumiza wananchi.”

Habari kuhusu kuhusu pendekezo la kuanzisha kwa ushuru wa VAT kwa mkate na maziwa ilitolewa na Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u.

Kulingana na Profesa Ndung’u kuondolewa hatua ya serikali kusaza bidhaa hizo dhidi ya utozaji wa ushuru wa VAT imefaidi matajiri kwa kiwango kikubwa kuliko masikini.

Endapo pendekezo hilo litapitishwa, bei ya mkate na maziwa inatarajiwa kupanda kuanzia Julai 1, 2024.

Hii ni kwa sababu wafanyabiashara wa bidhaa hizo sasa hawatadai kurejeshewa ushuru unaotozwa malighafi ya kutengeneza bidhaa hizo. Watalazimika kuelekeza gharama hiyo kwa watumiaji wa bidhaa hizo ambao ni wanunuzi.

Akiongea wakati wa mahojiano yaya hayo, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alisema pendekezo hilo linaashiria wazi kwamba serikali ya Kenya Kwanza haijali hali ngumu inayowakabili Wakenya.

“Waziri Ndung’u anadai kuwa mkate na maziwa ni bidhaa zinazotumiwa kwa wingi na watu matajiri. Mbona anasahau kuwa watu matajiri ndio wachache mno nchini Kenya?” akasema Bw Sifuna ambaye pia ni Katibu Mkuu wa ODM.

Seneta huyo alisema kuwa asilimia 70 ya wakazi wa Nairobi ni maskini ambao tegemeo lao kuu ni bidhaa kama vile maziwa na mkate.

“Mnamo Jumatano niliona ripoti iliyosema kuwa ni asilimia tatu pekee ya Wakenya ndio wanaopokea mapato ya Sh50,000 kwenda juu. Je, utawaita wata hawa tabaka la matajiri?” Bw Sifuna akauliza.

Seneta huyo aliahidi kuwaagiza wabunge wa mrengo wa Azimio kupinga ushuru huo ambao unawaumiza mahasla.

Pia mbunge wa Rangwe Lilian Gogo (ODM) amepinga pendekezo hilo.