Habari Mseto

Mbunge wa Machakos amkejeli Murathe, asimama na Ruto

January 9th, 2019 1 min read

Na Stephen Muthini

MBUNGE wa Machakos Mjini, Bw Victor Munyaka amejiunga na kikundi cha viongozi wanaompigia debe Naibu Rais William Ruto kwenye azma yake ya Urais 2022.

Bw Munyaka ambaye alichaguliwa kwa tikiti ya chama cha Jubilee alisema, Bw Ruto ana haki ya kuwania kiti cha Urais kama Mkenya yeyote yule, kwa sababu Rais Uhuru Kenyatta haruhusiwi kisheria kuwania muhula mwingine wa kuongoza taifa.

Akizungumza katika soko la Mavinye ambapo alisambaza basari kwa wanafunzi kutoka familia maskini, Bw Munyaka alikosoa matamshi ya hivi majuzi ya aliyekuwa naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe, akisema yana hatari ya kusambaratisha chama hicho.

Aliyataja matamshi ya Bw Murathe kuwa ya kikabila.

“Murathe awache kutoa matamshi ambayo ni ya kikabila na ya kutawanya. Kenya ni nchi ya zaidi ya makabila 42 na sote twapaswa kuishi kwa amani na masikizano,” akasema.

Hata hivyo, alipokuwa akijiuzulu Jumapili, Bw Murathe alisisitiza kuwa atafika katika Mahakama ya Juu kumzuia Bw Ruto kuwania urais, kwa kuwa anaamini urais unajumuisha Rais na Naibu Rais.