NA SAMMY KIMATU
MBUNGE wa Mavoko, Bw Patrick Makau amesikitika kwamba Mahakama ya Juu ilitoa uamuzi wa kuzima Hazina ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF).
Akitetea hazina hiyo, Bw Makau amesema wenyeji wanategemea fedha hizo kufaidika na maendeleo mashinani.
Amezungumza hayo leo Jumanne baada ya kupiga kura yake katika kituo cha biashara cha Joska kilichoko mkabala wa barabara ya Kangundo.
Aidha, mbunge huyo ameambia Taifa Leo kwamba anaamini atawabwaga wapinzani wake zaidi ya 10 kutokana na rekodi yake ya kuchapa kazi.
Msimamizi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) katika eneo hilo, Bi Jane Wasirwa amesema katika vituo vyote vilivyo kwenye wadi nne katika eneo bunge la Mavoko, kila kitu kilikuwa shwari kimipangilio.
“Vituo vyote vya kupigia kura vilifunguliwa saa 11 asubuhi na kuongeza na wapigakura pamoja na maajenti wao walikuwemo kabla ya shughuli ya kupiga kura kuanza,” Bi Wasirwa akasema. Isitoshe, katika kituo cha Borehole kilichoko maeneo ya Syokimau, usalama ulikuwa umeimarishwa wapigakura wakichagua viongozi wao bila matatizo.
Zaidi ya hayo, wapigakura wakijitokeza kwa wingi katika shule ya msingi ya Mulolongo na hakukuwa na hitilafu zozote.
Na katika kituo cha kupigia kura cha NITA mkabala wa barabara ya Nairobi/Namanga, hali ilikuwa shwari.
“Jioni, kituo hiki cha NITA ndicho hutumiwa katika kujumlisha kura zote katika eneo bunge la Mavoko, Kaunti ya Machakos,” Bi Wasirwa akasema.
Ndani ya Shule ya Msingi ya KMC iliyoko mjini Athi River, wapigakura walipanga foleni kuanzia saa tisa za usiku wa kuamkia Jumanne.
Kwa ujumla, kituoni hapo hapakushuhudiwa jambo lolote la kuyumbisha uchaguzi.