Habari MsetoSiasa

Mbunge wa ODM amtetea Uhuru dhidi ya kejeli za wabunge wa Jubilee

January 8th, 2019 1 min read

Na VALENTINE OBARA

MBUNGE wa Rarieda, Dkt Otiende Amollo, amemtetea Rais Uhuru Kenyatta dhidi ya viongozi wa Jubilee kutoka Mlima Kenya wanaodai rais amepuuza eneo hilo kimaendeleo.

Dkt Amollo alisema malalamishi ya wabunge hao wanaojumuisha Moses Kuria (Gatundu Kusini), Kimani Ngunjiri (Bahati) miongoni mwa wengine hayana msingi kwa kuwa kikatiba, wabunge wana mamlaka zaidi kuendeleza maeneo yao kuliko rais.

“Tulibadilisha mfumo wa uongozi uwe kwamba rais hadhibiti ugavi wa raslimali tofauti na ilivyokuwa zamani. Kwa hivyo kama kuna kosa, ni wabunge wanafaa kulaumiwa,” akasema kwenye mahojiano katika runinga ya NTV mnamo Jumanne asubuhi.

Viongozi kadhaa wa eneo la kati na Mlima Kenya wamekuwa wakidai utawala wa Rais Kenyatta unajishughulisha zaidi kuendeleza maeneo mengine huku akisahau ngome zake kuu za kisiasa.

Miongoni mwa miradi iliyogusiwa ni ujenzi wa barabara na kilimo.

Hii ni licha ya kuwa Naibu Rais William Ruto amekuwa akizuru maeneo hayo mara nyingi kuzindua miradi ya maendeleo, na vile vile serikali iliingilia kati kusaidia wakulima wa kahawa na miraa.

Dkt Amollo alieleza kuwa kile kinachodhaniwa kuwa misaada kwa wakulima wa mahindi na miwa maeneo ya magharibi si misaada kwani ni wakulima waliopeleka bidhaa zao kwa viwanda na maghala ya serikali ilhali hawakulipwa na wanadai haki yao.

Viongozi wengine wa Mlima Kenya walijitenga na wenzao wanaolalamika wakataka wamheshimu rais.

Miongoni mwa waliosuta wenzao kwa kumkosea heshima Rais Kenyatta ni Seneta wa Kaunti ya Murang’a, Bw Irungu Kangata, Kimani Wamatangi (Kiambu) na Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu.

Bw Kangata alisema ingawa kuna changamoto hapa na pale kimaendeleo, ukweli ni kwamba serikali imefanya iwezavyo kupeleka maendeleo maeneo tofauti ya nchi ikiwemo Mlima Kenya.

Seneta huyo, sawa na Bw Waititu, waliongeza kwamba wabunge wenyewe wana jukumu la kushinikiza serikali kuendeleza maeneo yao kupitia kwa njia za kiungwana badala ya kuanika malalamishi yao hadharani.