Habari MsetoSiasa

Mbunge wa zamani akwepa majukumu ya malezi

May 22nd, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

ALIYEKUWA mbunge wa Lamu Julius Ndegwa ameshtakiwa na mwanamke anayemtaka kugharamia maisha yake na mwanawe kwa kuwalipia kodi ya nyumba na kumlea mtoto, ambaye anadaiwa kumtelekeza.

Rehema Susan Maalim anadai kuwa mkewe Ndegwa, akiambia korti kuwa mbunge huyo wa zamani hajawalipia kodi ya nyumba kwa miezi kadhaa, wala kutuma pesa za kugharamia maisha ya mtoto wao.

Mwanamke huyo aidha ameeleza korti kuwa mbunge huyo wa zamani ambaye ndiye anafaa kulipa kodi kwa miezi mitano iliyopita hajakuwa akifanya hivyo, akisema anatishiwa kutimuliwa na mali yake kuuzwa.

Tayari mwanamke huyo amepata amri kutoka kwa mahakama ya watoto ya Tononoka, kumwelekeza Bw Ndegwa kulipa Sh140,000 ambazo mwanamke huyo anadaiwa za kodi ya nyumba, ili asitimuliwe.

Hakimu Mkuu Mkazi Lucy Sindani mwezi uliopita alielekeza Bw Ndegwa alipe deni la kodi hiyo, ambayo inahitajika na mmiliki wa nyumba ambapo Bi Maalim na mwanawe wanaishi, kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi hiyo.

Mwanamke huyo alifika kortini baada ya kupokea ilani mbili, ya kumtaka alipe kodi na nyingine ya kumtahatharisha kuwa mali yake itauzwa asipofanya hivyo.

Aliambia korti kuwa mbunge huyo wa zamani alitelekeza majukumu yake kwa kukosa kumshughulikia mtoto na kulipa kodi.

Alisema alikuwa akiishi katika nyumba ambapo alilipa Sh18,000 kwa mwezi lakini kiongozi huyo akamhamishia katika nyumba nyingine alikolipa Sh35,000, japo baadaye akatoweka.

“Aliacha kulipa kodi bila kunijulisha wala sababu zozote, wala kutupa pesa za kujikimu,” akaeleza korti.

Kesi hiyo itatajwa Jumatano, japo Bw Ndegwa hajajibu madai ya mkewe huyo.