Mbunge wa zamani wa Kaloleni afariki

Mbunge wa zamani wa Kaloleni afariki

Na Mohamed Ahmed

ALIYEKUWA mbunge wa Kaloleni, Gunga Mwinga alifariki jana akipokea matibabu katika hospitali moja jijini Mombasa.Kwa mujibu wa famili yake, kiongozi huyo alifariki baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Hata hivyo, familia hiyo haikufichua ugonjwa aliokuwa akiugua.Akizungumza na wanahabari, mjomba wa marehemu Bw Fredrick Kahindi, alisema kuwa Bw Mwinga aliaga dunia mwendo wa saa tisa usiku wa kuamkia Jumapili.

“Kama familia tunasikitishwa na kufiwa na kijana wetu ambaye alikuwa tumaini kuu kwetu. Kifo hiki ni cha ghafla kwani amekuwa hospitalini kwa muda mfupi tu,” akasema Bw Kahindi.

Ripoti zilieleza kuwa Bw Mwinga alifikishwa hospitalini mnamo tarehe 24 mwezi huu na kukosa kusherehekea sikukuu ya Krismasi na familia yake.

“Tutaanza mipango ya mazishi leo baada ya kukutana kama familia na kutoa taarifa baadaye kuhusiana na kuzikwa kwa marehemu,” akasema Bw Kahindi.

Bw Mwinga alikuwa mbunge wa eneo la Kaloleni kwa muhula mmoja kati ya mwaka wa 2013 na mwaka 2017 ambapo alishindwa na mbunge wa sasa Bw Paul Katana.Bw Katana jana aliungana na familia ya mwendazake hospitalini ambapo alitoa risala zake za rambirambi kwa familia.

“Wakazi wote wa Kaloleni wanaomboleza kwa kuondokewa na kiongozi aliyewahudumia. Alikuwa mshindani wangu lakini tulikuwa marafiki. Tumeshtushwa na kifo chake lakini tunaomba Mungu awape subira watu wa familia yake,” akasema Bw Katana.

Kifo cha Bw Mwinga ni miongoni mwa vya watu mashuhuri katika kanda ya Pwani waliofariki mwaka huu.Miongoni mwa watu hao ni wanasiasa wakongwe akiwemo aliyekuwa mbunge wa Changamwe Ramadhan Kajembe pamoja na wake zake.

Aliyekuwa mbunge wa Likoni Masoud Mwahima pia alifariki mwaka huu na baadaye kufuatiwa na mkewe wiki jana.Mbunge wa Msambweni Suleiman Dori naye alifariki mwaka huu tukio lililochangia kuwepo kwa uchaguzi mdogo katika eneobunge lake.

You can share this post!

CECIL ODONGO: Muungano wa Kalonzo hauna ushawishi kisiasa

LEONARD ONYANGO: Uchaguzi mdogo Nairobi ndio mtihani halisi...