Michezo

Mbungo aajiriwa kuinoa Rayon Sports ya Rwanda

February 27th, 2020 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

ALIYEKUWA kocha wa AFC Leopards, Andre Cassa Mbungo amesajiliwa na klabu ya Rayon Sports ya Rwanda.

Mbungo aliagana na Leopards mwishoni mwa mwaka uliopita baada ya klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kushindwa kumlipa mshahara wake kwa miezi kadhaa, huku naibu wake, Anthony Kimani akichukuwa usukani.

Leopards ilisajili Mbungo mnamo Februari 2019 kujaza nafasi ya Marko Vasiljevic aliyetimuliwa kufuatia matokeo duni yaliyoiacha timu hiyo katika nafasi mbaya wakati huo.

Alipowasili, Mbungo aliisaidia Leopards kupata matokeo mazuri na kurejea miongoni mwa saba bora kabla ya kuondoka.

Timu hiyo maarufu kama Ingwe kwa sasa inashikilia nafasi ya sita jedwalini baada ya kucheza mechi 21, lakini ingali na matumaini ya kutwaa ubingwa wa msimu huu, au kumaliza katika nafasi mbili za kwanza.

Mbungo ambaye pia aliwahi kuwa kocha wa Kiyovu Sports, AS Kigali na timu ya taifa ya Rwanda, aliondoka baada ya wachezaji kadhaa wa kigeni aliosajili kutoroka kwa kutolipwa kama yeye.

Amejiunga na Rayon ambayo kwa sasa inakamata nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu ya Rwanda ikiwa na pointi 41; saba nyuma ya vinara APR.

Wakati huo huo, Elvis Osok wa Posta Rangers amejumuishwa kwenye orodha ya wachezaji waliopigwa marufuku kucheza mechi za KPL wikendi hii.

Nyota huyo anajiunga na mlinzi wa Gor Mahia Joash Onyango ambaye pia aliikosa mechi yao dhidi ya Zoo Kericho na sasa hatakuwepo wikendi wakicheza na Western Stima.

Katika mechi hiyo, Western Stima nao hawatakuwa na Villa Oromchan ambaye alipigwa kadi nyekundu kwenye mechi ya awali.

Wachezaji wengine ambao watakaa nje wikendi hii ni Simon Abuko wa Kenya Commercial Bank (KCB) kutokana na kadi tano mfululizo za manjano.

Kwa sasa kocha wake, Zedekiah Otieno anatafuta mtu wa kujaza nafasi yake watakapokutana na Bandari FC katika mechi yao ya raundi ya 23.