Makala

MBURU: Matumizi ya pesa vyuo vikuu sasa yaanze kumulikwa

September 7th, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

MUDA umefika kwa serikali sasa kuanza kumulika jinsi vyuo vikuu vya umma vinatumia pesa ambazo vinapewa ili kufanikisha masomo ya juu, kufuatia habari za majuzi kuhusu madai ya wizi wa mamilioni ya pesa katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara.

Ripoti hiyo iliyopeperushwa na runinga ya Citizen Jumapili ilisema Naibu Chansela wa Chuo hicho amekuwa akiongoza ufujaji wa mamilioni ya pesa kujinufaisha kibinafsi, wakati chuo chenyewe bado kinakumbwa na changamoto.

Ni ukweli ulio wazi kuwa vyuo vikuu vya umma nchini vimekuwa vikikumbwa na matatizo mengi, hasa ya ukosefu wa pesa na rasilimali za kuwezesha masomo na utafiti kuendeshwa ifaavyo.

Matatizo haya, mara kwa mara, yamesababisha viwango vya elimu kudorora, vyuo kuwasomeshea wanafunzi madarasani tu, wakati mwishowe ‘wanafuzu’ bila kupata ujuzi wa moja kwa moja wa kazi wanazosomea.

Katika vingi vya vyuo vikuu vya umma nchini, wanafunzi kusoma hadi kumaliza bila kuwahi kushiriki tafiti za kisayansi, kiteknolojia ama zingine zinazowiana na kozi wanazosomea ni jambo la kawaida, hali ambayo imesemekana kuwa ni kutokana na uchache wa rasilimali.

Hii ni hali ambayo imehatarisha ubora wa elimu ya vyuo vikuu nchini.

Matatizo hayo ni kando na changamoto nyingine zinazovikumba kama migomo ya mara kwa mara ya wafanyakazi wakilalamikia mazingira mabovu kazini, na ya wanafunzi wanaponyimwa huduma muhimu ambazo zinafaa kutolewa.

Mara nyingi, kiini cha migomo hii huwa kukosekana kwa pesa za kufanya jambo fulani, ndipo waathirika wanaamua kutatiza huduma kama mbinu ya kupigania haki zao.

Serikali haina budi ila kuanzisha uchunguzi wa kina katika usimamizi wa vyuo nchini na kuunyoosha, ili wanafunzi na wafanyakazi wasiwe wakiteseka kila mara, wakati rasilimali zinaporwa na wasimamizi.

Inachukiza sana wakati maafisa ambao wamepewa jukumu la kulinda pesa za umma wanakuwa wa kwanza kuziiba, licha ya kuwa wanalipwa mishahara minono na kuwa kazi zao zinawahitaji kuwa waadilifu kwa kiwango kikubwa.

Serikali isimsaze yeyote anayepatikana na hatia ya kupora pesa, kwani matunda ya wizi huo yamekuwa kudorora kwa viwango vya elimu, na zaidi ya yote kuathiri uchumi wa taifa.