Makala

MBURU: Mswada ukifaulu utazima hospitali kuzuilia wagonjwa, maiti

September 27th, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

MSWADA wa marekebisho kwenye Sheria ya Afya, unaopendekeza serikali iwe ikitengea hospitali za umma Sh4.8 bilioni ili kuzuia visa vya wagonjwa na maiti kuzuiliwa, ni wa manufaa sana.

Mswada huo ambao uliwasilishwa na mbunge wa Nyando, Jared Okello umependekezwa wakati unaofaa kwani Wakenya wameteseka kwa muda mrefu.

Kwa miaka mingi, familia nyingi humu nchini, haswa zisizo na uwezo wa kifedha zimelalamikia hali ya hospitali kuzuilia wapendwa wao ambao wanashindwa kulipia matibabu, baada ya kutibiwa.

Hospitali nyingi bado hadi sasa zinaendelea kuzuilia watu ambao wamepata nafuu kwa kuwa wanadaiwa pesa za matibabu, huku waliofariki miili yao ikizuiliwa mochari.

Kuna baadhi ambao wameendelea kuishi hospitalini na kwa muda mrefu, na familia nyingine zikiomboleza pia kwa muda mrefu kwa kukosa namna ya kulipa bili za hospitali ili kuweza kupewa mwili wa mpendwa wao.

Serikali itafanya jambo la busara mswada huu ukifaulu kuidhinishwa, na hatimaye kuwa sheria, kwani ni hatua ambayo itawaokoa maelfu ya Wakenya ambao husalia bila namna ya kushughulikia hali inayowakabili.

Ni matumaini yangu- na ninaamini ya Wakenya wengi pia- kuwa bunge litaupitisha mswada huo kwa kauli moja, kwani wabunge wanaelewa fika matatizo ambayo familia nyingi hupitia.

Mapema 2019 Kamati ya Afya Bungeni ilikumbana ana kwa ana na uzito wa suala la hospitali kuzuilia watu na maiti, wakati ilifahamishwa kuwa hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) pekee ilikuwa imezuilia maiti 387 kwa lazima.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa KNH, Thomas Mutie pia aliambia kamati hiyo kuwa hospitali hiyo ilikuwa imewazuilia wagonjwa 184.

Hospitali ilikuwa ikidai familia za waliofariki Sh5.9 bilioni, na waliotibiwa na kupona Sh5.6 bilioni.

Visa hivyo vilipata kujulikana tu baada ya kumulikwa na vyombo vya habari, japo ni ugonjwa ambao umesambaa katika takriban hospitali zote nchini, maelfu ya familia zikilia.

Watu wengi nchini wanaishi kuomboleza kutokana na hali ya kufiwa na wapendwa wao, lakini wanakosa kuwazika kwa kuwa maiti zao zinaishia kuzuiliwa na hospitali.

Limekuwa suala tata kwani hospitali -hasa za kibinafsi zimekuwa zikijitetea kuwa haziwezi kuendelea kutoa huduma endapo zitakuwa zikitibu watu bure, huku zikisema zinadai watu mabilioni ya pesa.

Lakini pia sharti maisha ya mtu na haki zake ziheshimiwe kwa kutozuiliwa hospitalini, awapo hai ama maiti. Kupitisha mswada huu kutakuwa faraja kubwa kwa wananchi wengi.