Makala

MBURU: Uhuru, Ruto na Raila hawajajitolea kutetea raia

January 29th, 2020 2 min read

Na PETER MBURU

MPANGO wa Maridhiano (BBI) umekuwa ukisifiwa kuwa utakaohakikisha kuwa Wakenya wanaishi kwa amani na kupendana pamoja na kuzika uadui wa miaka mingi, hasa wa kikabila na kisiasa.

Kwa takriban mwaka mzima, jopo la BBI lilizunguka kote nchini kukusanya maoni ya Wakenya kuhusu wanapohisi panahitaji mabadiliko katika uongozi wa nchi.

Hadi sasa, wengi wameonekana kuunga mkono mapendekezo yaliyopo katika ripoti iliyotolewa na jopo hilo miezi miwili iliyopita, japo tangu kutolewa kwake, wanasiasa wa mirengo tofauti wamekuwa wakishiriki vita vya ubabe kuhusu BBI na sasa wanaelekea kuchafua zaidi juhudi zote zilizowekwa kuifanikisha.

Yalikuwa matumaini ya Wakenya kuwa mpango wa BBI haungeingizwa siasa na kuwa badala yake ungemwangazia Mkenya wa kawaida na mahitaji yake ya kimsingi kwanza, na kwa upana maslahi ya taifa.

Hata hivyo, kwa kuangazia matukio ambayo tumekuwa tukishuhudia ya wanasiasa kujibizana kuhusu mchakato huu mzima, ni wazi kuwa tayari wameuteka nyara na kuanza kujitafutia sifa na umaarufu kupitia BBI.

Cha kuhuzunisha ni kuwa sasa inaonekana kama kwamba maslahi ya Mkenya wa kawaida yamewekwa kando na ni viongozi wanaoshiriki vita vya ubabe, japo wakitumia jina la Mkenya ili kutoa taswira kuwa bado wanatujali.

Wanasiasa wamegeuza mikutano inayodaiwa ni ya kushauriana na wananchi kuhusu ripoti hiyo kuwa ya kupiga tu siasa zao na kuwashawishi raia kuunga mkono vipengele ambavyo vitawafaidi wao.

Jopo la BBI lilikuwa na fursa ya kuokoa taifa hili kutoka kwa minyororo ya uadui wa kikabila na kisiasa na vizuizi vingine vya umoja na kukua kwa taifa.

Lakini huenda juhudi hizo na mamilioni ya pesa zilizotengwa kufanikisha mpango huo zikapotea, endapo viongozi wa kisiasa wataendelea na tabia hii chafu.

Cha kuhuzunisha zaidi ni kuwa viongozi wa kitaifa kama Rais Uhuru Kenyatta, naibu wake William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga hawaonekani kama waliojitolea kutetea maslahi ya Mkenya wa kawaida katika suala hili kwa kuchukua msimamo thabiti. Badala yake wameacha wafuasi wao kuchafua hewa, wakati wao wenyewe wanapumbaza kuwa wako pamoja na Wakenya.

BBI ni mpango ambao una nia njema, na ambao sote tukijitolea kuufanikisha mambo kama vita vya kikabila, machafuko ya kisiasa na uadui wa kimaeneo nchini yatakuwa hadithi za kale.