Habari

Mbwa amjeruhi kibarua sehemu za siri

May 28th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MWANAMUME wa makamo anauguza majeraha mabaya ya sehemu zake nyeti baada ya kushambuliwa na mbwa wa kampuni moja ya Kahawa mjini Ruiru.

Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 38 ni kibarua katika kampuni ya kahawa ya Oakland Coffee mjini Ruiru.

Kulingana na maelezo yake ni kwamba mnamo mwishoni mwa wiki jana, alipofika katika eneo la kampuni hiyo askari anayelinda lango kuu aliachilia mbwa na kwa ghafla akamng’ata sehemu za siri huku akipata majeraha mabaya.

Wahudumu wa bodaboda wa eneo la Murera walilazimika kuandamana kuhusiana na tukio hilo.

“Sisi wanabodaboda tumekuwa tukidhulumiwa na askari wanaolinda kiwanda hicho. Wakati mwingine hata wanatukataza kuingiza wateja ndani ya kiwanda hicho,” alisema Bw Elias Mwangi ambaye ni mhudumu wa bodaboda.

Naye Kenneth Njuguna ambaye pia ni mhudumu anasema wamesumbuliwa kwa muda mrefu.

“Tunataka wakuu wa kampuni hiyo wajue wanastahili kuwachukulia askari hao hatua mara moja,” alisema Bw Njuguna.

Jirani wa mwathiriwa, Bw Francis Mwanzi aliyechukua jukumu la kumpeleka majeruhi hospitalini alisema mwanamume huyo alijeruhiwa vibaya.

Alisema alipelekwa Ruiru Level 4 halafu baadaye akatumwa Thika Level 5 kwa matibabu zaidi.

“Mimi kama jirani nilitumia fedha zangu ili kusimamia matibabu yake. Bado anastahili kuchunguzwa zaidi,” alisema Bw Mwanzi.

Mamake mwathiriwa ambaye ana umri wa miaka 57 alisema mnamo Jumatatu kwamba anahofia afya ya mwanawe kwa sababu alipata majeraha mabaya.

“Mimi sina chochote kifedha na jirani yangu ndiye aliyetusaidia,” alisema mama huyo.

Matibabu

Aliiomba kampuni ya Oakland Coffee ifanye hima kumsaidia mwanawe ili apate matibabu ya haraka.

Naye meneja mkuu wa kampuni ya Kofinaf Coffee ambayo ni kampuni mama kwa zingine tano kukiwemo Oakland, Bw Michael Gitau alisema hawajapata ripoti rasmi kuhusu tukio hilo, lakini wanaendelea kufanya uchunguzi ili kubainisha ukweli wa mambo.

Meneja mkuu wa kampuni ya Kofinaf Coffee, Ruiru Bw Michael Gitau, akihutubia waandishi wa habari afisini mwake Mei 27, 2019. Picha/ Lawrence Ongaro

“Iwapo tutapata kuwa mlinzi wetu alihusika na uovu huo bila shaka tutamchukulia hatua za kisheria,” alisema Bw Gitau na kuongeza wataendelea na matibabu yake hadi apate nafuu.

Alisema kampuni hiyo ina vitengo vingine vitano vikijumuisha wafanyakazi wapatao 8,000 ambao huchuna kahawa kwenye mashamba hayo.

Afisa mkuu wa usalama Bw Thomas Wekesa alisema watahakikisha mlinzi aliyehusika na jambo hilo anachukuliwa hatua ya kisheria.

“Sisi kama kampuni tunazingatia maslahi ya wafanyakazi wote bila ubaguzi ambapo hata tumewawekea bima kwa majeraha yoyote,” alieleza Bw Wekesa.

Alisema hawangetaka kuona jina la kampuni likiharibiwa bure lakini “tutahakikisha haki imetendeka kwake.”