Kimataifa

Mbwa ampiga risasi mwanamume

May 31st, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

IOWA, AMERIKA

MWANAMUME alishangaza wengi alipofichua jinsi alivyopigwa risasi na mbwa wake.

Bw Richard Remme, 51, ambaye ni mkazi wa eneo la Fort Dodge, Amerika, alisema alikuwa akicheza na mbwa wake nyumbani wakati mbwa alipofyatua risasi kutoka kwa bunduki yake na kumpiga mguuni.

Ripoti zinasema kwamba mwanamume huyo aliambia polisi walikuwa wakicheza kwenye kiti lakini akamrusha mbwa juu na anashuku aliporejea chini aligonga bunduki na risasi ikafyatuka kwa bahati mbaya.

Mashirika ya habari yalimnukuu kusema kwamba baada ya kufyatua risasi, mbwa huyo alilala kando yake na kuanza kulia alipotambua amefanya jambo baya.

“Nilikuwa nimelala kwenye kochi na tulikuwa tunacheza, mimi na mbwa wangu. Nilikuwa namrusha juu kutoka pajani mwangu na ninadhani aliangulia bunduki mara moja na alipogeuka, kidole chake kimoja kilifyatua risasi. Mbwa wangu alinipiga risasi,” akanukuliwa kusema.

Hata hivyo, jeraha alilopata halikuwa baya kwani alitibiwa akaruhusiwa kwenda nyumbani.