Mbwa apima corona kwa ufanisi mkuu

Mbwa apima corona kwa ufanisi mkuu

Na MASHIRIKA

HANOVER, Ujerumani

DAKTARI mmoja wa wanyama nchini Ujerumani amewafundisha mbwa wa kunusa (sniffer dogs) jinsi ya kugundua virusi vya corona katika mate ya mwanadamu, mbinu ambayo imeandikisha ufanisi wa kima cha asilimia 94.

Mbwa hao wamefuzwa kutambua “harufu ya corona” kutoka kwa seli za watu walioambukizwa, akasema daktari huyo kwa jina Esther Schalke. Anahudumu katika kitengo cha mbwa katika Chuo cha Kijeshi nchini Ujerumani.

Mbwa kwa jina Filou, asili ya Belgian Shepherd, mwenye umri wa miaka mitatu na mwenzake Joe Cocker, wa asili ya Cocker Spaniel, na mwenye umri wa mwaka mmoja, ni mbwa wawili wanaopokea mafunzo katika Chuo Kikuu cha Utabibu wa Wanyama, jijini Hanover.

“Tulifanya utafiti ambapo tulielekeza mbwa kunusa sampuli kutoka kwa wagonjwa wa Covid-19. Na tunaweza kusema kuwa wametoa matokeo yenye uhalisia wa kima cha asilimia 94,” akasema Hoger Volk, mkuu wa kliniki ya tiba ya wanyama.

“Kwa hivyo mbwa wanaweza kutawambua watu walioathiriwa na virusi vya corona na wale wasioathiriwa. Vile vile, wana uwezo wa kubaini wenye dalili za ugonjwa huo na wasio na dalili hizo,” akaongeza.

Waziri mkuu wa jimbo la Lower Saxony, Stephan Weil, alielezea kufurajishwa na utafiti huo. Hata hivyo, alipendekeza kuwa mbinu hiyo ifanyiwe majaribio zaidi ya mbwa wa kunusa kutumika kote katika jimbo hilo, ukiwemo mji wake mkuu, Hanover.

“Sasa tunahitaji kufanya majaribio zaidi katika hafla mbalimbali kote katika jimbo hili,” Weil akaeleza.

Nchini Finland, mbwa waliofunzwa kutambua virusi vya corona waliamba kunusa sampuli za wasafiri katika uwanja wa ndege wa Helsinki-Vantaa mnamo Septemba 2020.

Huo ulikuwa mpango wa majaribio ambao uliendeshwa pamoja na mbinu za kawaida za kupima virusi vya corona.

Usimamizi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Santiago pia umekumbatia matumizi ya mbwa kutambua waathiriwa wa Covid-19.

TAFSIRI NA: CHARLES WASONGA

You can share this post!

Shughuli zarejea kawaida baada ya shule iliyogeuza madarasa...

Ibrahimovic afikisha mabao 500 na kuongoza AC Milan kurejea...