Michezo

Mbwana Samatta ni andazi moto, amezewa mate na klabu nne za EPL

June 6th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MSHAMBULIAJI matata wa Tanzania, Mbwana Samatta yuko juu ya orodha ya silaha zinazotafutwa na klabu ya Brighton & Hove Albion kutoka Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika kipindi kirefu cha uhamisho kitakachofungwa Agosti 8, 2019, baada ya kufunguliwa Mei 16.

Samatta, 26, ambaye ni mchezaji wa Genk nchini Ubelgiji, pia anamezewa mate na mabingwa mara saba wa Uingereza Aston Villa, ambao watarejea katika EPL msimu ujao wa 2019-2020, washindi wa Uingereza msimu 2015-2016 Leicester pamoja na Watford na Burnley. Mabingwa mara tatu wa Ligi Kuu ya Italia AS Roma pamoja na washindi mara saba wa Ligi Kuu ya Ufaransa Olympique Lyonnais pia wako kwenye foleni ya kutafuta nyota huyu mwenye bei ya Sh1.5 bilioni.

Inasemekana Samatta yuko tayari kabisa kuhamia nchini Uingereza baada ya kung’ara sana katika Ligi Kuu ya Ubelgiji msimu 2018-2019.

Alipachika mabao 23 kati ya 63 yaliyofungwa na Genk na kusaidia klabu hiyo kushinda ligi kwa mara ya kwanza tangu msimu 2010-2011. Alitwaa kiatu cha Ebony, zawadi anayopata mwanasoka bora kutoka Bara Afrika kwenye ligi ya Ubelgiji.

Tuzo hii iliwahi kunyakuliwa na nyota Romelu Lukaku, Vincent Kompany, Michy Batshuayi, Marouane Fellaini, Emile Mpenza, Celestine Babayaro na Daniel Amokachi na wengineo.

Samatta ataongoza mashambulizi ya Tanzania katika Kombe la Afrika (AFCON) litakaloanza Juni 21 na kukamilika Julai 19 mwaka 2019 nchini Misri.

Kuondoka Genk

Alichangia mabao mawili katika kampeni ya Taifa Stars kurejea AFCON baada ya kuwa nje miaka 30.

Gazeti la Sun linasema kwamba baada ya AFCON kutamatika, Samatta anatumai kuondoka Genk, ambayo alijiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea miamba wa soka ya Afrika, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na kutua katika Ligi Kuu ya Uingereza.

Inasemekana Brighton imekuwa ikifuatilia soka ya Samatta kwa muda. Kocha wa zamani wa Brighton, Chris Hughton pia alikuwa shabiki mkubwa wa Samatta. Kocha mpya wa Brighton, Graham Potter pia anamheshimu sana mshambuliaji huyu kwa kazi yake safi.

Hata hivyo, si Brighton pekee imemtambua kuwa mchana-nyavu matata. Itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Aston Villa, Leicester, Watford, Burnley pamoja na klabu zingine barani Ulaya zikiwemo Roma na Lyon.

Katika AFCON 2019, Tanzania iko Kundi C pamoja na Senegal, Algeria na Harambee Stars ya Kenya ambayo inajivunia kuwa na mchezaji maarufu kutoka Afrika Mashariki, Victor Wanyama.