MBWEMBWE: Kiungo Di Maria ni mwenye guu la Almasi, ana magari na makasri ya kutisha

MBWEMBWE: Kiungo Di Maria ni mwenye guu la Almasi, ana magari na makasri ya kutisha

Na CHRIS ADUNGO

ANGEL Di Maria, 33, ni kiungo mvamizi raia wa Argentina ambaye kwa sasa anasakata soka ya kulipwa katika kikosi cha Paris Saint-Germain (PSG) nchini Ufaransa.

Mbali na kuwa kiungo, pia ana uwezo wa kuwajibishwa kama mshambuliaji na ni miongoni mwa mawinga wanaochukuliwa kuwa bora zaidi duniani.

Alianza kusakata soka kitaaluma akivalia jezi za Rosario Central kabla ya kuhamia Benfica akiwa na umri wa miaka 19 mnamo 2007.

Alisaidia klabu hiyo kutwaa taji la kwanza baada ya miaka mitano katika Ligi Kuu ya Ureno kabla ya kuhamia Real Madrid.

Aliongoza miamba hao wa Uhispania kunyanyua taji la La Liga na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kabla ya kuyoyomea Uingereza kuvalia jezi za Manchester United mnamo 2014 kwa rekodi ya Sh9.3 bilioni.

Hadi sasa akivalia jezi za PSG, Di Maria ametwaa mataji manne ya Ligue 1, matano ya Coupe de France na manne ya Coupe de la Ligue.

Alisaidia kikosi hicho kutinga fainali ya kwanza ya UEFA mnamo 2019-20 na ndiye wa nane kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote katika klabu hiyo.

Tangu awajibishwe na Argentina kwa mara ya kwanza mnamo 2008 akiwa na umri wa miaka 20, Di Maria amechezea mabingwa hao wa Copa America zaidi ya mechi 100.

Alifunga bao lililoshindia Argentina dhahabu ya Olimpiki mnamo 2008 na alikuwa sehemu ya kikosi kilichonogesha fainali ya Kombe la Dunia 2014 pamoja na Copa America 2015 na 2021.

Akisoma migongo ya Lionel Messi, Neymar na Kylian Mbappe wanaodumishwa na PSG kwa mishahara ya juu zaidi, Di Maria ndiye mchezaji wa nne ghali zaidi kambini mwa miamba hao wanaonolewa na kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur, Maurico Pochettino.

Kufikia sasa, mgongo wake kimshahara unasomwa kwa karibu na Gianluigi Donnarumma, Sergio Ramos, Mauro Icardi, Marquinhos na Achraf Hakimi.

UKWASI

Di Maria ni miongoni mwa wanasoka ambao miguu yao imewavunia magunia ya fedha katika ulingo wa soka.

Thamani ya mali yake kwa sasa inakadiriwa kufikia Sh7 bilioni na kiini kikubwa cha utajiri wake ni mshahara wa Sh18 milioni aliokuwa akipokezwa kwa wiki na miamba wa soka ya Ureno, Benfica kabla ya Real kumshawishi kutua uwanjani Santiago Bernabeu kwa kima cha Sh2.8 bilioni mnamo 2010.

Baada ya kuwatambisha Real kwa kipindi cha misimu minne, alihamia Man-United kwa mshahara wa Sh22 milioni kwa wiki.

Ingawa alifanikisha uhamisho huo kwa kutia saini mkataba wa miaka mitano, kushuka kwa kiwango cha ubora wake ugani ni kiini cha Man-United kumtia mnadani baada ya muhula mmoja.

PSG walimsajili kwa Sh6.6 bilioni na kumpokeza mkataba wa miaka minne ya kwanza mnamo Julai 2015.

Di Maria hujipa fedha nyinginezo za ziada kutokana na marupurupu na bonasi za kushinda mechi akivalia jezi za PSG na timu ya taifa ya Argentina.

Kwa mujibu wa Jorge Paulo Agostinho Mendes ambaye ni wakala wa Di Maria, thamani ya mteja wake kwa sasa imeimarika sana na kikosi kinachomhitaji lazima kiweke mezani Sh15 bilioni mwishoni mwa muhula huu.

Di Maria pia ni balozi wa kutangaza bidhaa za kampuni za Nike na Electronic Arts (EA Sports) ambazo humkabidhi zaidi ya Sh40 milioni kila mwezi.

MAGARI

Sawa na sogora yeyote wa haiba yake, Di Maria anamiliki magari mengi ya kifahari.

Miongoni mwa michuma anayoisukuma ni gari aina ya Audi Q7 lililomgharimu Sh24 milioni, Ferrari 458 ya Sh17 milioni na Range Rover Sport ya thamani ya Sh26 milioni.

Mchezaji wa PSG Angel Di Maria akionyesha mojawapo ya magari yake ya thamani kubwa. Picha/ Hisani

MAJENGO

Di Maria ambaye pia ni raia wa Italia, anamiliki jengo la kibiashara lenye thamani ya Sh600m katika eneo la Prestbury viungani mwa jiji la Cheshire, Uingereza.

Ana makasri mawili ya kifahari jijini Paris, Ufaransa, jingine la takriban Sh420 milioni jijini Rosario, Argentina na moja la thamani ya Sh300 milioni jijini Turin, Italia.

FAMILIA

Di Maria alizaliwa mnamo Februari 14, 1988 jijini Rosario, Argentina. Mnamo 2011, alifunga pingu za maisha na Jorgelina Cardoso, kichuna mzawa wa Argentina ambaye amekuwa mpenzi wake wa muda mrefu.

Kwa pamoja na mkewe, wamejaliwa mtoto mmoja wa kike, Pia, ambaye alizaliwa katika hospitali ya Universitario Monteprincipe, Uhispania akiwa na miezi sita pekee.

You can share this post!

UDAKU: Usicheze na Georgina, mapambo yake pekee ni bei ya...

Harambee Stars yarejea nyumbani na pointi moja kampeni ya...