Makala

MBWEMBWE: Yaani aisee huyu Hugo Lloris hudaka vyote vilivyo vizuri

October 5th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIPA matata wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya Ufaransa, Hugo Lloris ni miongoni mwa walinda-lango wanaodumishwa kwa mshahara mnono katika kikosi cha kocha Jose Mourinho.

Usogora wa Lloris mwenye umri wa miaka 33 umemkweza hadhi miongoni mwa makipa wanaohemewa sana na vikosi maarufu vya bara Ulaya, China na Amerika.

Kwa sasa, anashikilia nafasi ya nane kati ya makipa ghali zaidi duniani katika orodha inayoongozwa na Alisson Becker (Liverpool), Kepa Arrizabalaga (Chelsea), David De Gea (Manchester United), Manuel Neuer (Bayern Munich), Marc-Andre ter Stegen (Barcelona), Ederson Moraes (Man-City) na Jan Oblak (Atletico United).

Mgongo wa Lloris unasomwa kwa karibu na Thibaut Courtois (Real Madrid) na Bernd Leno (Arsenal).

UKWASI

Kufikia mwishoni mwa mwaka jana, majarida ya The Richest na Celebrity yalikadiria thamani ya mali ya Lloris kufikia kima cha Sh5.8 bilioni. Kiini kikubwa cha pato lake ni mshahara wa yapata Sh88 milioni ambao anapokezwa na Hotspur mwishoni mwa kila mwezi.

Mbali na ujira huo ambao unafikia takriban Sh22 milioni kwa wiki, Lloris hujirinia hela nyinginezo kutokana na marupurupu ya kusajili ushindi na sare katika ngazi ya klabu na timu ya taifa mtawalia.

Malipo hayo yanamweka katika orodha ya masogora wanaodumishwa kwa gharama ya juu zaidi kambini mwa Hotspur wakiwemo Harry Kane, Son Heung-Min na Erik Lamela.

Wachezaji wengine wanaodumishwa kwa mshahara wa juu kambini mwa Tottenham ni pamoja na Dele Alli, Moussa Sissoko na sajili mpya Tanguy Ndombele aliyesajiliwa kutoka Olympique Lyon ya Ufaransa kwa kima cha Sh7.8 bilioni.

Mojawapo ya sababu za kuongezeka kwa kiwango cha gharama ya matumizi ya Tottenham katika kipindi cha misimu miwili iliyopita hadi kufikia Sh18 bilioni kwa mwaka ni unono wa mshahara wa nyota hawa, hasa Lloris, Kane na Son ambao pia hujipa mafungu manono ya riziki kutokana matangazo ya kibiashara kutoka kwa kampuni mbalimbali ambazo zimewafanya kuwa mabalozi wa mauzo wa bidhaa zao.

MAGARI

Lloris hana tofauti kubwa na wachezaji wa kufu yake walio na uhakika wa kutia kapuni kitita kinono cha pesa kutokana na usogora wao uwanjani. Ingawa anamiliki magari mengi, mawili anayoyapenda zaidi ni Audi A6 lililomgharimu Sh18 milioni na Mercedes Benz AMG lenye thamani ya Sh20 milioni.

Mkewe huendesha gari aina ya Ferrari 458 ambalo lilimgharimu Lloris kima cha Sh25 milioni mnamo 2015.

MAKASRI

Lloris anamiliki jumba la kifahari lenye thamani ya Sh600 milioni jijini London, Uingereza anakoishi na familia yake akiwa kazini. Ana kasri jingine la haiba kubwa jijini Nice, Ufaransa alikozaliwa mnamo Disemba 26, 1986.

MAPENZI NA FAMILIA

Lloris ni mumewe kichuna Marine aliyeanza kutoka naye kimapenzi wakati wakiwa bado wanafunzi wa shule ya upili. Waliamua kula yamini na kuihalalisha ndoa yao kupitia harusi waliyoifunga mnamo Julai 2012 jijini Nice, Ufaransa katika sherehe za kufana zilizohudhuriwa na Meya wa jiji hilo, Christian Estrosi.