Na WANGU KANURI
MCHESHI MC Jessy, ambaye anafahamika kihalisia kama Jasper Muthomi, amekiasi chama cha Devolution Empowerment (DEP) kinachoongozwa na Gavana wa Meru, Kiraitu Murungi na kujiunga na chama cha UDA.
Akitetea msimamo huo kupitia ukurasa wake wa Instagram, Bw Muthomi alisema kuwa ushawishi wa watu kutoka eneo bunge la Imenti Kusini ndio ulimfanya kubadilisha msimamo.
“Nilipopata simu kutoka kwa ‘Hasla’ Dkt William Ruto akinikaribisha katika chama hicho, ilibidi nitii wanachotaka watu wangu. Ni vizuri kujiunga na timu itakayoshinda,” akaandika.
Mcheshi huyo ambaye anapania kumrithi Kathuri Murungi ambaye ndiye mbunge wa eneo bunge la Imenti Kusini hivi sasa, alitangaza nia yake ya kuwa kwenye kinyang’anyiro mwaka jana.
Akiidhinishwa na baadhi ya wazee kutoka Igoji, Bw Muthomi alipokezwa silaha za kiasili kama ishara ya kumuunga mkono anapowania kiti cha ubunge.
Japo ni mara yake ya kwanza kuwa kwenye kinyang’anyiro cha kisiasa, umahiri na umaarufu wake katika ulingo wa sanaa ndicho kigezo chake.