Habari Mseto

MCA adaiwa kumtia adabu mgema kwa kukataa kumuuzia mvinyo

June 5th, 2018 1 min read

Na Waikwa  Maina

MFANYABIASHARA mjini Ol Kalou, Kaunti ya Nyandarua anauguza majeraha anayodai yalitokea kwa kupigwa na diwani kwa kukataa kumuuzia pombe.

Mwathiriwa, Gathairu Gathairu alivunjika mkono mbali na majeraha mengine. Mpwawe, aliyekuwa amefika kumsaidia, naye alipata majeraha madogo.

Bw Gathairu alisema alifika katika baa yake mwendo wa saa tano usiku ili kufanya hesabu ya mauzo ya siku hiyo.

Hata hivyo, alimpata Bw Mburu wa Maria, ambaye ni diwani, akiwahangaisha wahudumu wake kwa kutomuuzia pombe, licha ya wakati wa kufunga baa kufika.

Diwani huyo anadaiwa kujaribu kuingia katika eneo la kuuzia kwa nguvu, hali iliyoanzisha mapigano.

Hata hivyo, diwani huyo amejitetea vikali, akisisitiza kwamba aliondoka katika baa hiyo kabla ya saa nne usiku.

Taarifa za polisi zinaeleza kwamba mwathiriwa alifika katika Kituo cha Polisi cha Ol Kalou saa tano usiku kuripoti kisa hicho.