Makala

MCA Tricky alia kukosa demu wa ‘kishua’  

January 7th, 2024 1 min read

NA RAJAB ZAWADI

MCHEKESHAJI MCA Tricky anadai umaarufu wake licha ya kumjalia baraka sufufu, pia umemleta nuksi hasa kwenye upande wa mapenzi.

Mvunja mbavu huyo anadai kwamba kwa sababu ya kuwa maarufu, ameshindwa kuwa kwenye mahusiano sahihi kwa sababu kila demu anayemtongoza anakuwa na mtazamo kuwa kwamba yeye ni jamaa anayetaka kumtumia kisha amhepe.

“Kero yangu kubwa ni suala la nyie watu kutuchukulia sisi watu maarufu kama vile tabia zetu sote ni moja. Imekuwa kwamba kila nikijaribu kumtongoza demu ambaye kikweli nimempenda kwa dhati, jambo la kwanza humjia akilini ni kwamba nimekuja kumcheza kisha nimtoke maana ndio imekuwa mtindo ya wasanii wengi. Jambo hili, mtazamo huu umenitesa sana kwa kweli maana ninaweza nikawa nimetulia sehemu nikamwona mrembo mzuri tu ambaye ninahisi atanifaa ama tunaendana ila nashindwa kumtongoza kwa kuhofia hayo niliyosema,” MCA Tricky kafungua moyo.

Staa huyo anasisitiza kuwa kwa umri ambao amefikia, amekuwa akitamani sana kuwa kwenye mahusiano yenye tija lakini imekuwa ngumu sana.
MCA Tricky aliwahi kuwa kwenye mahusiano na kidosho Reena mwenye asili ya Ethiopia ambaye aliishi kumposti sana kabla ya kuacha kufanya hivyo na tetesi ni kwamba walishaachana jambo ambalo mcheshi huyo hukwepa kulizungumzia.

Maselebu wengi, hasa wale maarufu wamekumbatia mbinu ya kuchapisha wachumba wao mitandaoni.

Watumiaji mitandao, huwa hawasahau na mambo yanapokwenda mrama intaneti hiyohiyo inatumika kuwachamba.